WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka
wasomi nchini kuondoa hofu ya kutumia fursa zilizo nje ya Tanzania
zikiwemo za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ile ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuomba na kufanya kazi za kujiletea
maendeleo.
Akizungumza katika Mahafali ya 48 ya
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam, Pinda alisema
inashangaza kuona wananchi wa nchi jirani wakinufaika na nafasi za
ajira zilizopo hapa nchini wakati Watanzania wana hofu ya kutafuta ajira
katika nchi hizo jirani.
Alisema serikali imeendelea kudumisha
ushirikiano na nchi jirani za Afrika Mashariki na SADC na kukubaliana
kuondoa vikwazo vya kiuchumi, jamii na kibiashara ili kuwezesha wananchi
kunufaika zaidi na fursa zilizopo katika kanda hizo.
“Wakati umefika kwa Watanzania kujenga
dhana ya kujiamini na kushiriki kikamilifu katika kuwania nafasi na
fursa zilizopo katika jumua hizi. Watanzania tunaweza, jambo la muhimu
ni kuamua na kuthubutu.
“Nitumie fursa hii kuwahimiza wahitimu
muombe kazi hata zilizo nje ya Tanzania, msifungwe na mipaka, fuateni
taratibu kujinufaisha na kulinufaisha Taifa,” alisema.
Akizungumzia umuhimu wa elimu ya
biashara, Pinda alisema Serikali ingependa kuona wawekezaji wengi wa
Kitanzani wakiwekeza kwenye rasilimali za mbalimbali nchini ikiwamo
gesi, madini, kilimo, lakini hilo halitawezekana kama hakutakuwa na
wasomi waliobobea kwenye fani hizo.
Alisema kwa kutambua fedha zinazotengwa
katika sekta ya elimu kuhusu biashara hazitoshi, alisema Serikali
itaendelea kuwekeza katika elimu ya biashara ili wananchi wengi waweze
kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi hasa biashara.
Katika hatua nyingine, Pinda aliwataka
Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya
makazi kushirikiana kuhakikisha wanawaondoa wavamizi wa eneo la CBE kwa
mujibu wa sheria.
Source: Habarileo
0 Comments