Tathmini
ya ujumla iliyofanywa na waandishi wetu karibu mikoa yote
ilikopiya oparesheni M4C na Pamoja Daima iliyoendeshwa na
viongozi hao wakuu wa CHADEMA pamoja na washirika wao kwa
siku 14, imeonyesha kwamba Zitto Kabwe bado ni ngangari sana
kisiasa....
Hali
hiyo imewalazimu viongozi hao sasa kutumia vitisho dhidi ya
wanachama na wafuasi wa chadema wanaopinga uamuzi wa kumvua
nafasi zake zote za uongozi mbunge huyo wa kigoma kaskazini....
Kwa
muda wa takribani siku 14, chadema kiliendesha operesheni M4C
Pamoja daima kwa kutumia nguvu na zana zake ilizo nazo, kwa
maana ya gari, pesa na helkopta kwa lengo la kuwafikia karibu
wanachama wao wote na mashabiki wote, operesheni iliyotafsriwa
na wachambuzi wa mambo kuwa ililenga kumwaga sumu ya
kumwangamiza Zitto Kabwe kisiasa....
Katika operesheni hiyo, chadema walitumia helkopita tatu ambazo wataalam wa mambo ya anga wanaweka wazi kuwa ni usafiri wa gharama kubwa ambao umekigharimu chama hicho kulipa takribani sh. milioni 57.6 kwa siku, sawa na sh. milioni 806.4 kwa siku zote hizo 14 za operesheni M4C , bila kuweka gharama nyingine kama vile posho kwa washiriki wa operesheni hiyo pamoja na mafuta ya magari, vipuri na matengenezo yake yaliyokuwa yakitumiwa na maofisa wengine wa chama hicho mikoani....
Chadema katika opresheni hiyo kilijigawa katika makundi manne, yalioongozwa na watendaji wa makao makuu ambao ni Mbowe, Dr. Slaa,mwanaseheria wa chama, Tundu Lissu na makamu mwenyekiti wa chadema ( zanzibar ) Said Issa Mohammed....
Timu ya Dr. Slaa ilipangwa kufanya mashambulizi katika mikoa ya nyanda za juu kusini, timu ya Mbowe ilielekea kanda ya ziwa wakati timu ya Lissu ilielekea mikoa ya kanda ya kaskazini na ile ya Issa Mohammed ilielekea mikoa ya magharibi mwa Tanzania kwa maana ya Kigoma, Tabora na Katavi....
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ilikokuwa timu ya Mbowe pamoja na Kigoma, Tabora na Katavi ilikokuwa timu ya Mnyika na wenzake, chadema kinaelezwa kuambulia aibu tupu baada ya vijana wengi wa chama hicho, wakiwemo baadhi ya viongozi kuwapokea watendaji hao wa makao makuu kwa mabango yaliyokuwa yakiwauliza "Zitto yuko wapi?"... "Zitto mnamuonea".
Habari kutoka Geita kwa mfano,zinasema mshituko alioupata Mbowe baada ya kupata mapokezi madogo tofauti na aliyotarajia pamoja na zomea zomea ya vijana wa chadema kesho yake wakati anaelekea Ngara na Biharamuro ulisababisha msafara wake kupata ajali katika harakati zake za kukwepa hasira za vijana hao wa chama chake....
Aidha, habari zinasema hasira hizo za vijana wa CHADEMA,waliokuwa wamejipanga barabarani wakiwa na mabango, zilimlazimisha Mbowe kukatisha ziara yake kanda hiyo ya ziwa na kuamua kukimbilia Iringa mjini ambako walau kuna vijana wachache wenye hasira na chama hicho kwa sasa....
Lakini pia, habari zinasema,mshituko huo wa Mbowe uliotokana na hali mbaya ya chama hicho kisiasa katika ukanda huo wa ziwa,ulikilazimisha chama hicho kumtaka katibu mkuu wake, Dr. Slaa ambaye alikuwa afanye opresheni M4C yake katika mkoa mzima wa Mbeya na wilaya zake, kukatisha ziara ndani ya mkoa huo na kuelekea Shinyanga, Geita na Mara kama moja za kuokoa jahazi....
Hata hivyo, pamoja na kupelekwa Dr. Slaa katika mikoa hiyo,bado vijana hao wa chadema wanaopigania mabadiliko walikataa kusalimu amri, na hasa baada ya wanafunzi wa elimu ya juu katika shule ya Sekondari ya Shycom kumpokea katibu mkuu huyo aliyepanga kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wao wa michezo, kwa mabango yaliyokuwa na maandishi yasemayo.."Zitto mmemuonea"
"Mabango yaliyompokea Dr. Slaa wakati anatua na helkopta yake katika uwanja wa Shycom, uliamsha hasira zake na kuanza kufoka ovyo jukwaani na kusema kama kuna mtu hapa anamuona Zitto Kabwe ndiye chadema basi amfuate yeye, sisi chama chetu hakimzuii, ruksa kuungana naye.",anaeleza shuhuda wa mapokezi hayo ya Dr. Slaa katika uwanja huo wa Shycom, ulioko mkoani Shinyanga...
Habari kutoka katika duru za vyuo vikuu vya elimu ya juu nchini, na hasa chuo kikuu cha Dar es Salaam, chuo kikuu cha Dodoma, chuo kikuu cha Tumaini Iringa,Mzumbe na Sokoine vyote vya Morogoro, zinasema karibu wasomi wote katika vyuo hivyo wamekatishwa tamaa na maamuzi ya kamati kuu ya chadema, ya kumvua nafasin zote za uongozi Zitto Kabwe, pamoja na kuwavua nafasi za uongozi Dr. Kitila Mkubo na Samsoni Mwigamba...
Kwa mujibu wa habari hizo kutoka katika duru za elimu ya vyuo vikuu, wasomi hao wamekataa kukubaliana na hoja ya usaliti unaodaiwa kufanywa na Zitto Kabwe na wenzake hao dhidi ya chama hicho, wakiweka wazi kuwa kiini cha mgogoro wote huo wa sasa ni "Vita ya demokrasia dhidi ya udikteta wa Mbowe na dr. Slaa"
Gazeti la Tazama Tanzania limeambiwa na watu waliokaribu na Mbowe na Dr. Slaa kuwa operesheni M4C Pamoja Daima, ilibuniwa na viongozi wakuu hao wa chadema baada ya mikakati yao ya awali ya kutaka kummmaliza kabisa kisiaa Zitto Kabwe kugonga mwamba....
Baadhi ya mikakati ya Mbowe na Dr. Slaa inayodaiwa kushindwa kupunguza kama si kumaliza kabisa nguvu ya Zitto Kabwe kisiasa ndani ya chama hicho, inaelezwa kwamba ni waraka uliosambazwa na makao makuu ya chadema ukidaiwa kutoka kwa Zitto uliowataka wenyeviti wa wilaya wa chama hicho kukiasi chama hicho, huku pia waraka huo ukidaiwa kuwataka watendaji hao wa wilaya kuishinikiza kamati kuu ya chadema kuitisha kikao cha baraza kuukujadili rufani ya Zitto...
Mikakati mingine ni ile iliyowataka viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho kutompa ushirikiano wowote pindi mwanasiasa huyo atakapoamua kufanya ziara ya kujibu mashambulizi dhidi yake yanayotoka kwa watendaji hao wa makao makuu wakiongozwa na mbowe na dr. Slaa...
Inaelezwa pia kwamba baada ya mikakati yote hiyo kushindwa kufua dafu kwa Zitto,ikiwemo operesheni hii ya hivi karibuni ya M4C pamoja daima,chadema wamebuni fitina na mizengwe mingine inayoonesha kwamba Zitto ametengeneza DVD zenye hotuba zake zinazojibu madai yote ya viongozi wake hao kuhusu usaliti...
"Nakuhakikishia kwamba viongozi wakuu wa chadema hawamuwezu huyu kijana.Watamaliza rasilimali zao zote, lakini mwisho wa siku Zitto ataibuka ngangari tu.Umewaona sasa baada ya kushindwa mbinu zao zote wameamua kutengeneza DVD ya kugushi hotuba zake",anasema kiongozi mmoja wa makao makuu ya chadema na kuongeza:
"Wameanza kutapatapa wakidai kwamba CCM wanataka kugharamia Zitto kwa kumkodishia Zitto Helkopta ili apite kote ilikopita operesheni M4C pamoja daima kujibu mapigo.Wote huu ni uzushi tu wakutaka wanachama wenzake wa chadema na wale wote waliokuwa na matumaini na chadema wamchukie Zitto.
"Lakini nakwambia Zitto si mjinga.Kisiasa ndani ya chadema, Zitto amewatangulia Mbowe na Dr. Slaa, hivyo hawatamuweza kamwe, labda kama wanataka kuua chama chao wagawane mbao kama akina Marando na Mrema walivyoua NCCR-Mageuzi"
Hata hivyo,habari kutoka kwa watu wa karibu na Zitto zinasema mwasiasa huyo amejipanga kuanza ziara ya kuzunguka maeneo yote ambako Mbowe na Dr. Slaa walipita kumwaga sumu ya kisiasa dhidi yake...
Kwa mujibu wa habari hizo, Zitto Kabwe atakuwa na timu ya wabunge wa chadema wasiopungua 10 ambao wanadaiwa kuwa na msimamo tofauti na Mbowe na Dr. Slaa kuhusu madai ya usaliti wa Zitto kwa chama chake...
"Alipaswa kuwa ameanza ziara hiyo, nadhani kilichomchelewesha ni ratiba ya vikao vya kamati za bunge.
Kuna orodha ya wabunge 9 ambayo inasema iko tayari kwa lolote ambao atakuwa nao katika ziara hiyo ya kusafisha sumu iliyomwagwa dhidi yake, lengo ni kutaka wanachama wenyewe waamue ni nani yuko sahihi katika mgogoro huu", anasema kiongozi mwingine wa chadema ambaye huko nyuma aliwahi kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na kambi ya mrema wakati wa mgogoro wa chama hicho...
Credit: Tazama Tanzania
0 Comments