
Padri Dennis Wigira wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
akihubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu
Joseph, Dar es Salaam jana.
Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Samwel Mshana
akizungumza katika ibada ya Ijumaa Kuu, alisema haoni nuru ya kupatikana
kwa katiba bora nchini.
Mshana alisema kuwa ana mashaka huko mbeleni Taifa
litaletewa katiba itakayowagawa Watanzania katika matabaka, jambo
ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
“Mimi kama kiongozi wa dini sina matumaini kabisa
ya kupata katiba ambayo itatufanya tuwe kitu kimoja, naona ni katiba
itakayowalinda wachache kwa misingi ya matabaka,”alisema.
Alisema katiba ndiyo mkombozi wa wanyonge, lakini
kwa jinsi mchakato unavyoendelea ni hofu na mashaka makubwa na
inaonekana kuna siri nzito ndani ya vyama vya siasa.
“Ndiyo maana wanavutana ili kuhakikisha itikadi na
masilahi ya vyama vyao yanaingizwa katika Katiba Mpya, hatukutegemea
wajumbe wawe na itikadi na misimamo ya vyama vyao vya siasa bila kujali
maslahi mapana ya Watanzania”.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es
Salaam, Eusebius Nzigilwa aliwaasa viongozi waliopo madarakani
kutowaonea watu wanaoonekana kuwa tishio kwa tawala zao.
“Wapo viongozi ambao wanaishi kama watawala wa
Kiyahudi waliomuua Yesu Kristo kwa sababu tu walimwona ni tishio kwao,”
alisema Nzigilwa na kuongeza kuwa wanyonge wanabambikiziwa kesi wakati
ndiyo wanaohitaji msaada wa kisheria.
Mchungaji Charles Mzinga wa Kanisa la KKKT, Azania
Front jijini Dar es Salaam alisisitiza kuwa upendo ndiyo kinga kwa
jaribu linalomkuta Mkristo popote alipo katika maisha ya hapa duniani.
Kwa upande wake, Padri Dennis Wigira wa Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam alilaani tabia ya
baadhi ya viongozi waadilifu katika Serikali kukosa uadilifu katika
serikali kuonekana hawafai kwa kuwa hawajaiba mali ya umma na kuishi
maisha ya kawaida.
Alisema wizi umekithiri kwa watendaji wa umma hivi sasa kiasi kwamba ambaye hafanyi anaonekana mjinga.
0 Comments