Mkuu shirika la habari la serikali SABC, Hlaudi Motsoeneng aliyepewa msichana kama zawadi
Uchunguzi umeanzishwa nchini Afrika Kusini kuhusu
madai kuwa mkuu wa shirika la habari la SABC alikabidhiwa msichana
mwenye umri wa miaka 23 kama zawadi.
Tume inayohusika na maswala ya usawa wa kijinsia, imesema kuwa
imepokea malalamiko kwamba viongozi wa kitamaduni walimkabidhi Mkuu
shirika la habari la serikali SABC, Hlaudi Motsoeneng mke kama zawadi.
Viongozi hao walikuwa sehemu ya kikundi cha wazee wa kitamaduni
waliokuwa wanataka vipindi zaidi vya lugha yao kupeperushwa kwenye
televisheni hiyo.
Serikali imesema kuwa tabia hiyo ni ya kuchukiza sana na kwamba inajuta jambo kama hilo lilitokea.
‘Wazazi walikubali’
Tukio hilo linasemekana kutokea wakati wa ziara ya hivi karibuni ya
Hlaudi Motsoeneng katika mkoa wa Limpopo Kaskazini mwa nchi hiyo ambako
yeye na maafisa wengine wakuu walikutana na wazee hao.
Taarifa ya serikali ilisema, ”Tabia ya kutumia wanawake kama zawadi
na kufafanishwa na mifugo wanaotolewa kama zawadi wakati msichana
anapooleka ni utamaduni usio kubalika na ni kinyume na haki za binadamu
na pia ni kama matusi kwa demokrasia na uhuru wa watu. ”
Takriban wasichana 10 waliorodheshwa mbele ya maafisa hao huku wakitakiwa kuchagua.
‘Alichagua aliyempendeza’
Bwana Hlaudi Motsoeneng alichagua mwanamke mmoja ambaye alimfurahisha.
“wasichana wote waliambatana na wazazi wao. Wazazi walifahamu kilichokuwa kinaendelea na inaarifiwa kuwa wote walikubali.
Kwa mujibu wa jarida Sowetan, bwana Motsoeneng alichagua msichana aliyekuwa na umri wa miaka 23 ambaye pia ni mwanafunzi.
Alipigwa picha akiwa kifua uchi akisimama kando yake.
Pia inaarifiwa alikabidhiwa Ng’ombe na Ndama.
Wizara ya maswala ya wanawake nchini humo, ilisema tabia hiyo ni hujuma kwa utamaduni
“tabia ya kutumia wanawake kama zawadi ungedhani ni n’gombe, bila
shaka ni hujuma kwa utamaduni, ” ilisema taarifa ya wizara hiyo.
Msemaji wa kituo cha SABC, Kaizer Kganyago, aliambia BBC kuwa
hajapokea habari yoyote kuhusu uchunguzi unaofanywa na tume hiyo na
kwamba ikiwa ina swali lolote kuhusiana na tukio hilo, inapaswa kuhoji
viongozi hao wa kitamaduni.
Lakini msemaji wa tume hiyo, Javu Baloy naye aliambia BBC kuwa ujumbe
tayari umewasilishwa kwa wote waliohusika na mapendekezo ya dhabu
yatatolewa mwezi ujao.


0 Comments