
BAADA
ya kujaribu kuficha migogoro nyuma ya kichaka cha Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), hatimaye bundi wa migogoro ameibuka tena ndani ya
CHADEMA.
Kwa
muda mrefu sasa, kumekuwemo mvutano kutokana na kile kinachodaiwa
ukiukwaji wa Katiba na matumizi mabaya ya madaraka na fedha za chama.
Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya viongozi wakiwemo wa ngazi za juu kuvuliwa uanachama na wengine kutimuliwa.
Baadhi
waliovuliwa uongozi ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na
aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Hata
hivyo, juzi wanachama wakiwemo wajumbe wa mkutano mkuu wa CHADEMA,
walitoa tamko zito wakiutuhumu uongozi wa juu kwa ubadhirifu wa fedha za
ruzuku na matumizi mabaya ya madaraka.
Pia
leo wanatarajia kuandamana kwenda katika Ofisi ya Msajili wa Vyama
Siasa nchini, kuwasilisha malalamiko hayo yakiwemo madai ya ufisadi na
ukiukwaji wa Katiba ya CHADEMA.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya CHADEMA, zilieleza kuwa malalamiko hayo yatafikishwa katika ofisi za msajili leo.
Awali,
malalamiko hayo yalikuwa yapekelekwe jana lakini ilishindikana kutokana
na Msajili (Jaji Francis Mutungi) kutokuwepo ofisini.
“Jana
malalamiko yalitakiwa kupelekwa lakini imeahirishwa hadi leo. Lakini
tunaiomba ofisi ya msajili iitake CHADEMA iitishe mkutano wa
wanachama,’’ alisema mmoja wa wanachama hao.
Uamuzi
wa wanachama hao, kupeleka malalamiko katika ofisi ya msajili ni
kutokana na chama hicho kushindwa kuitisha mkutano wa baraza kuu la
chama hicho kama kanuni zinavyotaka.
Katibu
wa CHADEMA mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Athumani
Balozi, alisema chama kimeshindwa kuitisha mkutano wa baraza kuu
kinyume cha katiba.
Alisema
Katiba inaagiza kila baada ya miezi 12, Baraza Kuu liitishwe, ambapo
lilipaswa kuitishwa kabla ya Februari, mwaka huu, lakini uongozi umekaa
kimya.
“Chama kimeshindwa na hata wanachama wanapohoji wanashindwa kupewa majibu ya kina juu ya lini mkutano utaitishwa,’’ alisema.
Alisema
CHADEMA inapokea zaidi ya sh. bilioni 10 za ruzuku kutoka Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini bado imeshindwa kujiendesha na hata
kukosa kitega uchumi.
Balozi
alisema wanahitaji mkutano wa baraza kuu, ili kuwataka viongozi wao
wakuu, Freeman Mbowe (Mwenyekiti) na Katibu Mkuu, Dk. Willbrad Slaa,
kujipima na kujiuzulu nyadhifa zao.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CHADEMA, John Mnyika,
alipoulizwa kuhusu madai ya wajumbe hao, alijibu yuko bungeni na
kuelekeza atafutwe Ofisa Habari wa Chama hicho, Tumaini Makene.
Hata
hivyo, Makene alipoulizwa aliomba apewe dakika tano ili aweze kutoa
majibu, lakini alishindwa kufanya hivyo na kila alipopigiwa simu yake
iliita bila majibu.
Credit: Gazeti la Uhuru
Credit: Gazeti la Uhuru
0 Comments