Wakati
mume wa mwimba Injili Bongo, Flora Mbasha, Emmanuel Mbasha akiachiwa
huru kwa dhamana kufuatia kesi ya kudaiwa kumbaka shemejiye, Mchungaji
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima ameibuka na kunena mazito kuhusiana na sakata hilo.
Mbasha
aliachiwa kwa dhamana juzi akitokea Gereza la Keko, Dar baada ya
kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya
Ilala, Juni 17, mwaka huu na kusomewa mashitaka mawili ya ubakaji ambayo
hata hivyo, aliyakana.
ILIVYOKUWA KORTINI
Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mheshimiwa Wilbeforce Luago siku
hiyo ya Juni 17, alitoa hoja kwamba upande wa jamhuri hauna pingamizi
hivyo dhamana ipo wazi.
Alisema
mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili, mfanyakazi wa serikali
na wa kutoka katika taasisi inayotambulika sanjari na shilingi milioni 5
kila mmoja. Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo siku hiyo hadi
hadi juzi alipotimiza, akaachiwa.
Mwendesha
mashitaka wa mahakama hiyo ambaye ni wakili wa serikali, Nassoro Katuga
bila kuchelewa aliitaja kesi hiyo yenye namba CC/186/2004 ambapo rafiki
wa Mbasha aliyejitambulisha kwa jina la George Mushi na baba wa
mtuhumiwa aitwaye Mwahimu Juma ndiyo waliofanikisha dhamana hiyo. Kesi
yake itatajwa tena Julai 17, 2014.
GWAJIMA SASA
Akizungumza
na mwanahabari wetu juzi wakati Mbasha akiwa nje kwa dhamana, Mchungaji
Gwajima alieleza namna ambavyo sakata hilo limeitikisa Injili nchini
Tanzania kutokana na kuibuka kwa madai mengi likiwemo suala la Flora
kusemekana amehamia nyumbani kwake kitu ambacho alikipinga.
Mchungaji Gwajima
Gwajima alisema anasikitika sana kuona ndoa ya Flora na Emmanuel Mbasha inatikisika akizingatia Flora ni muumini wake hivyo moja kwa moja ugomvi wao unaonekana kutia dosari mwenendo mzima wa uinjilishaji katika jamii.
“Naumizwa
sana na sakata hili lakini hivi karibuni niliamua kuwaita ndugu wa
pande zote mbili (Flora na Mbasha) nikazungumza nao kwa kirefu na
tukamaliza tofauti zote lakini tatizo likabaki lile la kisheria zaidi
(mashitaka ya ubakaji kwa Emmanuel),” alisema Gwajima ambaye makao makuu ya kanisa lake yapo Kawe jijini Dar.
AANDAA TAMKO ZITO
Mchungaji
Gwajima alisema kutokana na sakata hilo kugusa Injili, ameandaa tamko
zito ambalo atalitoa rasmi atakaporudi safari yake ambayo hakueleza
anakokwenda.
“Hatuwezi kukaa kimya juu ya hili, nasafiri lakini nikirudi tu nitatoa tamko rasmi kwa kuwaalika waandishi wa habari,” alisema.
IBADANI JUMAPILI
Katika
hatua nyingine, ndani ya ibada ya kanisa hilo iliyofanyika Jumapili
iliyopita, Mchungaji Gwajima alitumia dakika kama 15 katika mahubiri
yake kutupa kile kilichodaiwa kuwa ni jiwe gizani ambapo wengi waliamini
ni kuhusiana na sakata hilo.
“Mimi
siyo kama wale, sijibu hoja kama zile, mfano ukiwa unaoga halafu chizi
akachukua nguo zako na ukamkimbiza nani ataonekana chizi? Tatizo la
Watanzania ni kuwa wakisikia kitu kipya kinaanza kwao badala ya
kukithamini wanakididimiza ili kisiendelee, lakini mimi siyo kama wao,” alisema.
Aliongeza: “Mimi
kila mwaka naenda Japan na ninawa-lecture Wajapani ambao pia huja hapa
kanisani zaidi ya 40 kila mwaka na mwaka huu watakuja Septemba, lakini
Watanzania hawashtuki na kuja kujifunza juu ya ufufuo wa wafu wengi wao
wanakalia kuandika stori kwenye magazeti lakini mimi siyo kama wale.”
AMEFUNGUKIA SAKATA LA MBASHA?
Ingawa
Mchungaji Gwajima hakueleza moja kwa moja kuhusu tukio la Mbasha lakini
maneno hayo yalitafsiriwa kwamba ni ya kujibu hoja zinazomhusisha yeye
na tukio hilo.
Anaendelea:”Mimi
nimehubiri nchi zaidi ya 53 duniani na nyingi za Ulaya na Marekani
halafu mtu amekaa Magomeni miaka yote anatengeneza stori ya gazeti,
unatarajia niijibu, mimi siyo kama wale nimetumwa na nina kazi natakiwa
kuifanya duniani na siwezi kufa mpaka niimalize.”
“Inawezekana
mlishawaangamiza wengi kabla ya mimi, kwa kuwatungia stori hizo za
uongo lakini mimi siyo kama wale na mwezi huu wa nane ninaendelea na
mkutano Iringa, waache waandike lakini mimi ni chombo kingine na siyo
kama wale.”
DONGO GIZANI?
Baadhi
ya waumini waliokuwa katika ibada hiyo, walibaki njia panda na katika
giza nene ingawa wengi waliamini alitupa vijembe katika sakata la Mbasha
haswa alipokuwa akisema, ‘mimi siyo kama wale’.


0 Comments