Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema itawachukulia hatua za kisheria
wamiliki wa klabu za usiku zinazokiuka maadili kwa kuruhusu klabu zao
kupiga ngoma ya ‘bunyerobunyero’.
Ngoma
hiyo iliibuka na kuwa maarufu hasa jijini Dar es Salaam baada ya Polisi
kupiga marufuku ngoma ya ‘kantangaze-kigodoro’ na ‘khanga moko’.
Onyo hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema ngoma hiyo imeibuka karibuni na inaenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Alisema
ngoma hizo hazina tofauti kubwa na vigodoro isipokuwa wahusika wa
‘bunyerobunyero wametofautisha maeneo ya kupinga ngoma hiyo ambayo ni
kwenye klabu za usiku tofauti na vigodoro ilikuwa ikipigwa mitaani.
“Tutahakikisha
kwa kushirikiana na halmashauri za miji pamoja na polisi kuhakikisha
hizi ngoma za ‘bunyerobunyero’ tunazipiga marufuku, kwasababu zinakiuka
maadili,” alisema Kova.
Alisema
Polisi imetoa onyo mara nyingi kuhusu ngoma hizo na kwamba hatua
inayofuata sasa ni kuwakamata wachezaji na wahudhuriaji wa ngoma hizo
pamoja na kuwakamata wamiliki wa klabu hizo na kuwapiga faini na
kuzifungia klabu hizo.
“Onyo hili linatolewa kwasababu hizi ngoma zimeenea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam,” alisema.
Kamanda
Kova alisema ngoma hizo zimetawaliwa na udhalilishaji wa hali ya juu
jambo linalochangia kuporomoka kwa maadili, hivyo hawatalifumbia macho.
“Uchunguzi
kwasasa unafanyika na endapo itabainika ngoma hizo kuendelea kuchezwa
basi Jeshi la Polisi na halmashauri za miji zitachukua hatua mbalimbali
za kisheria ikiwa ni pamoja na kuzifungia klabu hizo kwasababu zinakiuka
taratibu za leseni,” alisema.

0 Comments