Mkazi
wa Singida Mjini, Jacqueline Kweka (30) jana alipandishwa mahakamani
mjini Hai akikabiliwa na tuhuma za kumfanyia ukatili mfanyakazi wake wa
ndani (15).
Inadaiwa
kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akimpiga mfanyakazi wake huyo sehemu
mbalimbali za mwili ikiwamo kumvuta nyama za sehemu za siri kwa kutumia
bisibisi.
Baada
ya tuhuma hizo kuibuliwa na raia wema, mtuhumiwa huyo alitoroka kutoka
Singida na kukimbilia kijiji cha Narumu wilayani Hai, Kilimanjaro
alikokamatwa baada ya taarifa kuvuja.
Mtuhumiwa
huyo alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi, Mfawidhi wa Wilaya,
Denis Mpelembwa na kukanusha mashitaka dhidi yake. Hati ya mashtaka hayo
ya kujeruhi mfanyakazi wake huyo ni ya awali ili kuruhusu polisi kutoka
Singida kwenda kumchukua mtuhumiwa huyo.
Akimsomea
mashitaka, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta Marwa Mwita alidai
mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo Julai mwaka huu siku tofauti.
Mtuhumiwa
huyo alikanusha mashitaka hayo na amerudishwa rumande hadi Agosti 21
wakati ukisubiriwa utaratibu wa kumsafirisha kwenda Singida.
Msichana
anayedaiwa kufanyiwa ukatili huo, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Hai kwa matibabu na taarifa zinadai amepoteza uwezo wa kusikia na
hapati tena siku zake za hedhi na amelazwa hapo kwa wiki ya pili sasa.
Hivi
karibuni matukio ya kunyanyasa wafanyakazi wa ndani yamezidi kushika
kasi likiwamo lile la msichana, Yusta Lucas (20) anayedaiwa kuteswa kwa
kung’atwa na kuchomwa kwa pasi mwili mzima na mwajiri wake Amina Maige,
mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Mwanamke
huyo ameshtakiwa kwa kosa la kumjeruhi mfanyakazi wake huyo kwa
kumng’ata sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia majeraha makubwa.
Kesi
hiyo ambayo imeendelea kuvuta hisia za watu wengi kila iitwapo,
inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar
es Salaam.
Baadhi ya watu wanaozungumzia unyanyasaji wa aina hiyo, wanataka upigwe vita na jamii.
0 Comments