
Familia ya
Bwana Sata wameiambia BBC kuwa Rais wa Zambia, Michael Sata, amefariki
dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika hospitali ya London alikokuwa
akitibiwa ugonjwa ambao haujatajwa.
Kifo chake kimetokea siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.
Mwanasiasa
huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza
chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye
alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party
Democracy, kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.
Michael
Chilufya Sata alizaliwa mwaka 1937 katika mji wa Mpika, eneo ambalo
lilikuwa wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya
madhehebu ya Katoliki, alifanya kazi kama afisa polisi, mfanyakazi wa
reli na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa
kikoloni. Baada ya Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani
mjini London, akiwa mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na
kampuni ya teksi.
Akiwa mwenye
sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo ya kuvuta sigara kwa muda mrefu,
Bwana Sata aliibuka katika siasa na kupata umaarufu katika miaka ya
1980.
Haraka
akapata sifa ya kuwa gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati
akiongoza jimbo la Lusaka na mtu wa utekelezaji kwa vitendo.
Lakini pia
alijulikana kama mtu wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki na mkali-
na wapinzani wake walisema jina alilopewa la bandia la "King Cobra"
alikuwa anastahili kuitwa hivyo.
Kwa mara ya
kwanza alionekana kama mtu ambaye angetekeleza ahadi za kupambana na
rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira na kuleta ustawi wa jamii.
Lakini kipindi chake madarakani kiligubikwa na kuuzima upinzani wa
kisiasa na kudorora kwa uchumi.
Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani.
0 Comments