Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya
Waziri Mkuu mstaafu,
Cleopa Msuya amemshauri Rais Jakaya Kikwete kupuuza matatizo
madogomadogo yanayojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba badala yake
asimamie uamuzi ya Bunge hilo ili kupata Katiba ambayo itaongoza nchi
kwa amani.
Msuya alisema hayo mbele ya Rais Kikwete jana
wilayani Mwanga, Kilimanjaro wakati wa hafla ya kumuaga baada ya
kung’atuka katika shughuli za kisiasa, iliyoandaliwa na CCM wilayani
hapa.
“Majibizano yanayotokea huko Dodoma kwa sasa
katika mchakato wa Katiba yasikukatishe tamaa, simamia uamuzi sahihi
ambao utalipeleka Taifa kwenye amani na utulivu,” alisema Msuya.
Pia aliishauri CCM kuhakikisha inarudi chini na
kuwa karibu na wananchi, ili kufanikiwa katika malengo yake na kutoa
mahitaji kwa wananchi pale yanapohitajika.
“Hivi karibuni tumeshuhudia viongozi wakitafuta
uongozi kwa kutoa rushwa ili waingie madarakani, ni vyema
viongozi wakachaguliwa kwa hiari na siyo kwa kutumia fedha,” alisema
Msuya.
Alisema viongozi wa namna hiyo ndiyo wanaolipeleka
taifa pabaya na hatimaye kuleta mkanganyiko katika chama hasa nyakati
za uchaguzi.
Alimpongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kwa kujituma katika kukihudumia chama
hicho kiasi cha wananchi wengi kurudisha imani.
Akihutubia katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema
katika miaka yake 29 ya kukihudumia chama na Serikali, Mzee Msuya
amewaachia Watanzania mambo mengi ya kuigwa.
Alisema kitendo cha chama kumuaga na kuelezea
wasifu wake, ni heshima ya kipekee ambayo wamempa kutokana na kazi
nzuri alizofanya katika Serikali na Taifa kwa ujumla.
“Mzee Msuya naomba muda huu unaokwenda kuungana na
wazee wenzako huko Usangi, uutumie kuandika kitabu ambacho utaachia
Taifa kama wasia wako, maana wewe unaifahamu hii nchi vizuri,” alisema
Rais Kikwete.



0 Comments