Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi, Isaya
Mngulu akikata utepe kuzindua ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013
Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba walioandaa ripoti
hiyo.
Matukio ya vyombo vya dola kutumia nguvu kupita kiasi yamezidi
kuongezeka nchini na kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka
2013 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), watu 34 waliuawa na
watumishi wa vyombo hivyo katika nyakati tofauti.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana inaonyesha kuwa
mauaji hayo yalitekelezwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi
la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na sungusungu. Vyombo vingine
vilivyotajwa katika matukio hayo ni polisi jamii na askari wa
Wanyamapori. Pamoja na matukio hayo, pia askari wanane waliuawa na raia
katika vurugu mbalimbali zilizohusisha pia kuvamiwa kwa vituo vinne vya
polisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema matukio hayo
yameongezeka kutokana na vyombo husika kutowachukulia hatua maofisa wake
baada ya kutekeleza mauaji.
Hata hivyo, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Erick
Komba alisema jana kuwa baadhi ya askari wa jeshi hilo waliobainika
kutekeleza vitendo hivyo walichukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu. Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mungulu
alisema watatumia ripoti hiyo kujirekebisha zaidi katika utekelezaji wa
shughuli mbalimbali za polisi.
Maeneo ya mauaji
Dk Bisimba alisema sehemu kubwa ya mauaji hayo
yalitokea katika matukio baina ya askari na wananchi pia kupitia
operesheni zilizotekelezwa na Serikali hususan Operesheni Tokomeza.
“Mambo makubwa matatu ndiyo yalikuwa na uvunjifu
mkubwa wa haki za binadamu; Operesheni Tokomeza na Kimbunga pamoja na
vurugu za gesi mkoani Mtwara,” alisema.
Alisema uvunjifu huo wa amani pia ulitokana na
matamko ya viongozi wa Serikali ikiwemo kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda bungeni Agosti mwaka jana, kwamba wananchi wanaovunja amani
wapigwe tu na vyombo vya dola.
Alisema mwaka 2013 kulikuwa na matukio ya kutisha
ya mauaji kwa mfano, watu kujichukulia sheria mkononi na kuua wengine.
Watu 1,669 waliuawa, ikiwa ni ongezeko la vifo 435 kutoka 1,234 mwaka
2012.
“Pia tulishuhudia aina mpya ya mauaji kama vile
kumzika mtu akiwa hai kwa imani potofu za kishirikina, kuwapiga mawe na
kuwachoma moto watuhumiwa... ni vitendo vya kutisha katika utoaji wa
adhabu ambavyo vinavunja haki za binadamu. Pia kumekuwa na ugumu kwa
upande wa polisi na waendesha mashtaka kufanya uchunguzi wa kina na
kuwashtaki waliotekeleza vitendo hivyo.”
Ripoti hiyo ya kumi na moja tangu zilipoanza
kutolewa mwaka 2002, pia imebainisha kuongezeka kwa vitendo vya kuwaua
watu kutokana na imani za kishirikina. Watu 765 waliuawa mwaka jana
ikilinganishwa na 630 mwaka 2012.
“Kati ya hao waliouawa wanawake walikuwa 505 na
wanaume 260,” iliongeza ripoti hiyo ikisema mikoa iliyokumbwa zaidi na
matukio hayo ni Geita, Mbeya, Shinyanga, Iringa, Tabora na Mwanza.
0 Comments