JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatarajiwa kufanya maonesho ya zana zake za kivita zinazotumiwa na askari wa nchi kavu kuanzia Julai 14 hadi 16, mwaka huu wakati wa kongamano kubwa la kijeshi ambapo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo nchini.
Kampuni zaidi ya 30 zinazotengeneza silaha na vifaa vya kijeshi kutoka ndani na nje ya nchi zitaonyesha bidhaa zao katika Kongamano hilo.
Akizungumzia kongamano hilo litakalofanyika kwenye
Ukumbi wa wa Milimani City, Dar es Salaam, Julai 14 hadi 16, mwaka huu,
mkuu wa kamandi ya Jeshi la Nchikavu, Meja Jenerali Salim Kijuu alisema
jana kuwa viongozi mbalimbali wakiwemo wadau wa jeshi watashiriki.
“Kampuni 32 za kimataifa zinazozalisha na kuuza
silaha na vifaa vya kijeshi zimethibitisha kushiriki katika maonyesho
hayo. Viwanda vyetu vya kijeshi na vile vya kiraia vinavyozalisha silaha
za kijeshi pia vitashiriki,” alisema Kijuu.
Alibainisha kuwa Tanzania itatumia fursa hiyo
kulitangaza jeshi lake katika jumuiya za kimataifa, hasa katika kipindi
ambacho linaelekea kwenye maadhimisho ya miaka 50 tangu lilipoanzishwa.
Alisema majeshi yatakutana kujadili jinsi ya
kukabiliana na changamoto za sasa za ulinzi na usalama hasa eneo la
Afrika Mashariki ambalo linakabiliwa na changamoto ya uvuvi haramu,
uharamia na jinsi ya kulinda maliasili za Taifa.
Brigedia Jenerali Simon Mumwi alisema ingawa
maonyesho hayo yanahusu silaha na zana za kijeshi, hayana lengo la
kuzitisha nchi jirani, bali kuimarisha uhusiano.
“Tunawaalika wenzetu ili waje tupeane ujuzi na
uzoefu wa changamoto za kiusalama na siyo kuwaonyesha kwamba na sisi
tupo,” alisema Mumwi.
Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya JWTZ Agosti, mwaka huu, kutafayika mazoezi makubwa ya kijeshi Arusha.
0 Comments