Advertisement

Responsive Advertisement

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA MAGOGO NA MATAWI YA MITI BARABARANI PINDI MAGARI YANAPOHARIBIKA


Serikali imewataka madereva wote nchini kuhakikisha wanatumia pembetatu ambazo zimeruhusiwa kisheria kuwekwa kama ishara pindi magari yao yanapopata hitilafu barabarani na si kuweka magogo, mawe ama matawi ya miti kama ishara. 
Akijibu swali la mbunge Hilda Ngoye bungeni Dodoma hii leo, Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mh. Pereira Silima amesema ni kosa kwa dereva kutumia matawi ya miti kama ishara kuwa gari lake limeharibika huku akionekana pia akikemea tabia ya madereva hao kuviacha vitu hivyo baada ya magari yao kutengemaa.
"Kuweka matawi ama mawe magogo barabarani ni kosa kisheria lakini ni kosa zaidi pale anapomaliza matengenezo ya gari lake anaacha vitu hivyo bila kuviondoa, kwa kweli hiyo huweza kupelekea matatizo zaidi ikiwemo ajali" amesema Waziri huyo. 
Amesema dereva anatakiwa kufuata sheria zinazowataka kuwa na pembetatu ambayo ni rafiki wa mazingira na si kukata matawi ya miti kwa kuwa yanachafua barabara na pia yanaharibu mazingira kwani miti hukatwa matawi. 
Baada ya majibu hayo mbunge wa Nkasi Mh. Ally Kessy amelazimika kumpa taarifa waziri huyo akimtaka kutozuia matumizi ya matawi ya miti kama ishara kuwa kuna gari limeharibika kwa kuwa matawi hayo husaidia kwa kiasi kikubwa.
Mh. Kessy amesema barabara nyingi zina kona na miteremko ama milima mikali na pindi gari linapoharibika katika mazingira hayo pembetatu haisaidii na badala yake matawi ya miti yanayowekwa barabarani yatasaidia kwa kiwango kikubwa huku akisisitiza madereva kuondoa matawi hayo baada ya magari yao kutengenezwa.
Waziri Silima ameipokea taarifa hiyo kwa kiasi fulani ingawa hakufafunia ni vitu gani amevipokea na ambavyo hajavipokea katika taarifa hiyo

Post a Comment

0 Comments