Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Zitto Kabwe
ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujieleza kwa kushindwa kesi
hadi kupoteza Sh340 bilioni za kodi ya ongezeko la mtaji katika
uchimbaji urani.
Juni 21, 2014 gazeti hili liliripoti hukumu ya kesi kati ya Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya JSC Atomredmetzoloto (ARMZ)
ikiituhumu kukwepa kodi ya zaidi ya Sh340 bilioni.
Mahakama ya Rufani za kodi ilitupilia mbali madai hayo ikiipa ushindi ARMZ.
Akizungumzia hukumu hiyo, Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, alisema jana kuwa kukosa kodi hiyo siyo upungufu wa sheria
bali ni uzembe wa Mamlaka ya Mapato na Wizara ya Nishati na Madini.
“Habari ya Serikali kukosa Sh340 bilioni za kodi ya ongezeko la
mtaji, imenigusa moja kwa moja kwa sababu mbili kubwa,” alisema na
kuongeza:
“Moja, Mwaka 2012 niliwasilisha muswada binafsi bungeni kurekebisha
Muswada wa Fedha 2012 ambao ulikuwa unabadili Sheria ya Kodi ya Mapato
2004 kwa lengo la kuweka vipengele vitakavyowezesha nchi kupata kodi
kutokana na mauzo ya kampuni za wawekezaji wanapouziana hisa au mali nje
ya nchi.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
“Pili, mwaka 2013 niligombana na Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo kuhusu suala la kodi kutoka Kampuni ya Mantra
Resources na Waziri alilihakikishia Bunge kuwa lazima kodi italipwa.
Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo wa TRA, Richard Kayombo alipoulizwa kwa
simu jana alisema asingezungumzia suala hilo Jumapili na kwamba suala
hilo bado lipo mahakamani.

0 Comments