JESHI
la Polisi limetangaza kuanzisha uchunguzi wa kina dhidi ya viongozi wa
kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliotajwa na
kada wa zamani wa chama hicho, Habibu Mchange, kujihusisha kupanga na
kutekeleza njama zenye mwelekeo wa ugaidi.
Limesema
tuhuma zilizotolewa na Mchange zimelishtua, hivyo zinapaswa kuchukuliwa
kwa uzito wa hali ya juu, unaohusisha mwenendo wa uchunguzi wenye
tahadhari wa makosa ya jinai, unaopaswa kuendeshwa na makachero
waliobobea kwenye kazi ya upelelezi.
Tamko
la kuanzishwa kwa uchunguzi huo limetolewa jana na Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, katika mahojiano na
MTANZANIA kupitia simu ya kiganjani alipotakiwa kutoa tathmini
iliyofanywa na polisi dhidi ya makundi mawili yenye uhasama wa kisiasa
yaliyoshutumiana hadharani kupanga na kutekeleza mauaji.
Mngulu
alisema ungamo la Mchange kuwa alishiriki kwa namna moja au nyingine
kupanga mipango ya mauaji, kuvuruga amani ya nchi na kulihusisha Jeshi
la Polisi na matukio ya mauaji aliyodai kutekelezwa na viongozi wa
Chadema, linaangaliwa kwa mitazamo miwili.
Alisema
mtazamo wa kwanza unaweza kuwa upotoshwaji unaofanywa makusudi ili
kuwahadaa polisi wasiendelee na uchunguzi wanaoufanya kuhusu matukio
hayo na kuanzisha mwingine mpya kulingana na tuhuma za Mchenge, na wa
pili madai hayo yanaweza kuwa na ukweli ambao utawaongoza makachero
kuwakamata wahusika halisi.
“Nilikuwa
sina taarifa, lakini sasa baada ya kuzipata ninafuatilia ukweli wa
kilichosemwa, lakini kumbuka wakati mwingine baadhi ya taarifa
zinazotolewa ni mbinu ya kukutoa kwenye mstari sahihi. Tuseme labda wewe
umeshamkamata Isaya anayetuhumiwa halafu mtu mwingine akajitokeza
akakuambia aliyefanya tukio ni John wakati kumbe lengo lake ni kukuondoa
kwenye mstari sahihi.
“Lazima
tuwe na tahadhari kwamba mtu huyu alikuwa wapi toka mwanzoni, kama yeye
alikuwa mtu mwema kwanini hakujitokeza mapema wakati tukio lilipotokea.
Niseme tu kwamba nikipata hiyo taarifa rasmi ya Mchange itanirahisishia
sana kazi,” alisema DCI Mngulu.
Alipotafutwa
jana na MTANZANIA kupitia simu yake ya kiganjani ili aeleze kama yupo
tayari kulisaidia Jeshi la Polisi kuthibitisha tuhuma zake kwa viongozi
wa Chadema, Mchange alisema tayari amekwishatoa ushahidi usiokuwa na
shaka, unaowapa polisi mahali pa kuanzia upelelezi wao.
Mbali
na ushahidi huo, alisema yuko tayari kushirikiana na jeshi hilo kueleza
na kutoa ushahidi wa kile anachokijua kuhusu madai aliyoyatoa, na
kuwataka polisi wamuite wakati wowote watakapohitaji msaada wake.
“Siyo tu kutoa ushahidi, nishautoa na niko tayari kuwaongezea taarifa na ushahidi mwingine nilionao wa kile nilichokieleza.
“Taarifa
yangu yenyewe ni ushahidi tosha, lakini wakati wowote niko tayari
kuwaongezea ushahidi na taarifa wanazozihitaji juu mauaji, niseme wazi
Mbowe (Freeman) ni muuaji mkubwa,” alisema Mchange.
TUHUMA ZA MCHANGE
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Tamali Hotel, Dar es
Salaam, Agosti 14 mwaka huu kwa lengo la kujibu tuhuma alizoelekezewa na
uongozi wa Chadema kuwa alishiriki kupanga njama za kulipua helikopta
iliyopangwa kuwabeba Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa na
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alisema ni madai ya kipuuzi
yaliyoratibiwa na Tundu Lissu.
“Haingii
akilini hata kidogo kwamba mimi nimepanga na CCM kuilipua helikopta
ambayo ingewabeba Dk. Slaa na Mnyika. Upuuzi huu ulioratibiwa na Tundu
Lissu, ni uthibitisho wa kushindwa na kuporomoka kisiasa kwa kasi ya
ajabu kunakoikabili Chadema kwa sasa,” alisema Mchange.
Katika
tuhuma nyingine, aliwataja Dk. Slaa, Lissu, Mbowe, Mnyika na Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa ndio mabingwa wa matukio ya kigaidi na
mauaji ya watu wanaotofautiana nao kimsimamo na mtazamo.
Mchange
aliyataja matukio aliyodai viongozi hao kushiriki kuyapanga na
kuyatekeleza kuwa ni pamoja na mauaji ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema,
Chacha Wangwe.
Tuhuma
nyingine ni kushiriki kikamilifu kupanga na kutekeleza mauaji
yaliyotokea mkoani Arusha pamoja na kumtumia kijana aliyemuelezea wajihi
wake kuwa ni mweupe, mwenye mazoea ya kufuga nywele nyingi,
aliyechanganya uraia wa Tanzania na Ujerumani kutekeleza matukio ya
kigaidi.
0 Comments