Gari
la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), lililokuwa likisafirisha
maiti 10 za watu kwenda katika Hospitali ya Mtakatifu Francis Ifakara,
wilayani Kilombero, limewagonga watu wawili waliofariki dunia papohapo,
eneo la Mtego wa Simba, Mikese mkoani Morogoro.
Waliokufa katika ajali hiyo iliyotokea saa 5:25 asubuhi jana ni dereva na abiria wa bodaboda.
Maiti
hizo zilizokuwa zimehifadhiwa katika mifuko maalumu ya plastiki,
zinaelezwa kuwa zilikuwa zikipelekwa katika Hospitali ya Mtakatifu
Francis, ili zitumike kwa mafunzo.
Akizungumzia
ajali hiyo katika eneo la tukio, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani
Mkoa wa Morogoro, Boniface Mbao alisema kuwa gari hilo lilikuwa
likiendeshwa na Pankrasi Pascal, mkazi wa Ifakara, wilayani Kilombero.
Mbao aliwataja waliokufa kuwa ni Shaaban Rajabu na Ally Benulo,
wakazi wa Kijiji cha Mikese, waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki.
Tukio
hilo limekuja siku kadhaa baada ya mabaki ya miili ya binadamu
kugunduliwa ikiwa imetupwa katika dampo moja lililoko Bunju, nje kidogo
ya Jiji la Dar es Salaam.
Chuo kimoja cha mafunzo ya udaktari wa magonjwa ya binadamu,
kilihusishwa na tukio hilo lililozua hofu kwa wakazi wengi wa jiji hilo.
Kamanda Mbao alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa
gari ambaye kwa sasa, anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
Kuhusu
maiti 10 zilizokutwa kwenye gari hilo, ofisa huyo wa polisi alisema
wanafanya mawasiliano ili kupata usafiri wa kuzifikisha katika Hospitali
ya Mtakatifu Francis, ilipokusudiwa.
Mashuhuda
wa ajali hiyo walisema chanzo ni mwendokasi wa dereva wa gari, huku
wakilalamikia kukithiri kwa ajali katika eneo hilo.
Walisema ajali hizo zimekuwa zikisababisha vifo vya watu wasiokuwa na
hatia na kwamba kuna haja Serikali kuweka matuta na vibao vya kuashiria
kona zilizopo eneo hilo.
0 Comments