Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani,
Papa Francis amekubali kumuondolea sakramenti ya upadri, Raymond Mosha
wa Jimbo Katoliki la Moshi ikiwa ni miaka 20 tangu padri huyo aombe
kuachana na daraja hilo.
Barua ya uamuzi wa Papa Francis ilisomwa
juzi katika parokia na vigango vyote vya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi
katika ibada zilizofanyika katika makanisa ya jimbo hilo.
Miongoni mwa parokia ambazo barua hiyo
ilisomwa ni Karanga ambako Paroko wake, John Matumaini alitoa tangazo
hilo katika ibada zote. Uamuzi huo ambao ni nadra kutolewa na Papa,
unamaanisha kuwa sasa padri huyo yuko huru kuoa na kuwa na familia.
Hata hivyo, wakati uamuzi huo
ukitangazwa rasmi juzi, tayari Padri Mosha ambaye ni profesa wa falsafa
na maadili katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha, ana mke na
watoto watatu ambao kwa sasa wako vyuo vikuu.
Padri Mosha alisema aliandika barua kuomba kuondolewa daraja hilo mwaka 1994 kabla ya uamuzi kutolewa juzi.
Katika orodha ya mapadre 185 wa Kanisa
Katoliki Jimbo la Moshi iliyopo katika tovuti ya jimbo hilo, jina la
Padri Mosha linaonekana likiwa ni namba 23.
Akizungumzia hatua hiyo, Padri Mosha
alisema: “Ninafurahi kufunguliwa kifugo hiki na hii itanifanya niishi
kama Mkristo. Kwa vile hawajaniondolea sifa ya kutoa huduma kama vile
ibada za mazishi, sakramenti ya mwisho na ubatizo, nitaendelea kutoa kwa
wahitaji kwa sababu ninaupenda ukristo.
“Nashukuru sasa nimekuwa muumini wa
kawaida nitaweza kufunga ndoa kanisani kwa kuwa nilikuwa nimefunga ndoa
ya kisheria tu kwa DC.”