
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji
Mbunge
wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji ameingia katika
mgogoro mpya baada ya kutuhumiwa kumpiga mbunge mwenzake kutoka
Tanzania, Dk Nderakindo Kessy jijini Nairobi, Kenya.
Bhanji,
ambaye amekuwa katika mgogoro na wabunge wenzake kwa kipindi cha miezi
miwili sasa, anadaiwa kumvamia Dk Kessy na kumpiga mgongoni.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Dk Kessy alisema tukio hilo lilitokea bungeni juzi jioni baada ya kikao kuahirishawa.
“Kwa
kuwa muda wa Bunge ulikuwa umeisha nisingeweza kuipeleka kesi hiyo
bungeni badala yake ikawa shambulizi na niliambiwa kiutaratibu
nikaripoti Kituo cha Polisi cha Bunge ambako baadaye nilikwenda na
kupatiwa cheti cha matibabu,” alisema Dk Kessy.
Alisema
baada ya kupatiwa cheti cha matibabu na polisi alikwenda katika
Hospitali ya AAR jijini humo ambako alipimwa na kupewa majibu
aliyoyapeleka polisi kwa uchunguzi.
Hadi tukio hilo linatokea, alisema hakuwa amekwaruzana na Bhanji zaidi ya kushangaa akimvamiwa.
“Baada
ya kunipiga hakukuwa na madhara ya papo kwa papo kama alama yoyote
mwilini au damu ila nayasikia maumivu, sijui hapo baadaye,” alisema
Mbunge huyo ambaye ni kada wa NCCR-Mageuzi.
Bhanji
hakupatikana jana kuzungumzia tuhuma hizo, kwani simu yake ilikuwa
imezimwa na hata ujumbe wa barua pepe alioandikiwa hakurudisha majibu.
Ofisa
Uhusiano Mwandamizi wa Eala, Bobi Odiko alisema: “Nimesikia kwamba
mmoja ya wabunge alimpiga mwenzake ‘kipepsi’ lakini ilikuwa nje ya
Bunge, bado ninaendelea kutafuta ukweli wa kina juu ya tukio hilo.”
Bunge
la Eala, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, limekuwa likitawaliwa na vioja
na mivutano ya hapa na pale na mikakati ya kumng’oa Spika Magreth Zziwa
kwa madai ya kutofanya kazi kwa weledi.
Hivi
karibuni, Bhanji aliliingiza Bunge hilo katika mvutano baada ya kudaiwa
kuliaibisha wakati wa ziara ya Ubelgiji iliyowashirikisha wajumbe wa
tume na wenyeviti wa kamati za Bunge hilo.
Alituhumiwa
kufanya fujo ndani ya ndege kwa kutoa lugha chafu kwa wabunge wenzake
na matamshi yasiyo ya staha katika hafla iliyoandaliwa na Balozi wa
Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala.
Baada ya tukio hilo, baadhi ya wabunge walitaka Bhanji achukuliwe hatua za kinidhamu.
Hali
hiyo ilifanya vikao vilivyokuwa vikifanyika jijini Kigali, Rwanda mwezi
uliopita kuahirishwa kila baada ya dakika 20 au 30 kutokana na wabunge
kutumia kanuni ya 31 kutoa hoja zao kutaka mjadala kuhusu Bhanji
ufanyike kwanza kabla ya kuendelea na kazi nyingine.
Bhanji
alikanusha tuhuma zote na kuziita uzushi na zenye nia ya kuzimisha
juhudi zake za kupinga njama ovu za kumng’oa Spika Zziwa.
Kabla
ya Bunge hilo kuanza Nairobi Novemba 14, Bhanji aliandika kwenye
ukurasa wake wa Facebook: “Kwa Tanzania kuna sahihi mbili tu… lengo
kubwa la kumwondoa Spika ni sehemu ya ‘mchezo mchafu ili kikundi fulani’
wamuweke Spika mwingine kwa masilahi ya wachache.”
Hata
hivyo, bado haijabainika wazi iwapo hatua ya kumvaa Dk Kessy ilikuwa ni
sehemu ya mvutano huo kwani Dk Kessy alisema hajui chanzo.
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wamepata taarifa za tukio hilo na
wamezipa umuhimu mkubwa na kimeshafikisha malalamiko rasmi kwa Waziri
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Mwenyekiti
wa wabunge wa Tanzania ndani ya Eala, Adam Kimbisa alisema hakuwa
ameambiwa chochote juu ya tukio hilo... “Nipo kwenye kikao. Sijaambiwa
chochote.” Alipoulizwa iwapo alikuwa na taarifa za awali juu ya tukio
hilo alisema: “Sina uhakika na habari hizo.”
Waziri
Sitta alikiri kusikia tukio hilo na kubainisha kuwa lilitokea kwa
bahati mbaya wakati Bhanji anapita katika kundi la wabunge na kumgonga
Dk Kessy na kwa kuwa alikuwa na haraka hakuweza kusimama.
Alisema Kwa kuwa Dk Kessy hakupata maumivu makali wabunge hao jana asubuhi walikaa pamoja na kuelewana.
Aliongeza
kuwa taarifa rasmi kutoka kwa naibu wake, Dk Abdallah Sadala aliyepo
Nairobi, ni kwamba baada ya maelewano hayo Sajenti wa Bunge alikwenda
kituoni hapo kueleza kwamba Bhanji hakufanya kitendo hicho kwa makusudi
na walikuwa wamemalizana.
via>>Mwananchi
0 Comments