MAKUBWA! Mke wa mtu aliyejitambulisha kwa jina
la Miinza Matoki (20), ameikimbia ndoa yake kisa kikielezwa kuwa ni
mauzauza ya kichawi anayokutana nayo.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Minza ambaye ni mkazi wa Manyoni
mkoani Singida alisema wazazi wake walimuozesha kwa ‘kibabu’ aliyemtaja
kwa jina moja la Samson ambaye aliwahi kuoa wanawake nane kabla yake
hivyo yeye kuwa wa tisa.
Alisema siku chache baada ya kuolewa alianza kuona mauzauza usiku
ambapo alidai alikuwa akichezewa mwilini na watu ambao hakuwafahamu
wenye sura za kutisha huku wakiwa wamevaa nguo nyeupe.
Mwanamke huyo alisema mchana alipokuwa akienda kuchunga ng’ombe
akirudi nyumbani alikuta kinyesi cha binadamu kwenye begi la nguo
zake.“Siku moja niliamshwa usiku saa kumi na kuambiwa niende kisimani
kuchota maji, nikakutana na mtu aliyevaa nguo nyeupe, nikamsalimia
hakuitika, nikachota maji na kuondoka, nilipotazama nyuma sikumuoana
nikaanguka na kupoteza fahamu.
“Nilijikuta nikiwa sehemu ambayo sikuifahamu, palikuwa na watu wengi
waliovaa nguo nyeusi ambapo nilishikwa mkono na mtu ambaye nilikuwa
namfahamu kwamba ni mtoto wa mjomba wangu, akanipandisha kwenye fisi
huku nikiwa nimevalishwa nguo nyeusi na kufungwa hirizi mwilini,
nikaamriwa nikamuue mama yangu na baada ya kupanda fisi tulienda kwa
mama yangu, mtu niliyeongozana naye alikuwa na utaalamu wa kutosha.
“Zoezi la kumuua mama lilishindikana ndipo nikaganda kwenye mlango na yule niliyeenda naye yeye aliondoka na kuniacha.
“Mama alipoamka asubuhi alinikuta mlangoni nikiwa sijielewi huku
nimevaa nguo nyeusi ‘kaniki’ na kufungwa hirizi, alimwita mganga
akanitoa pale na kuninywesha dawa lakini sikupona ndipo nikapelekwa kwa
mchungaji kuombewa.
“Baada ya hapo nilirudi kwa mume wangu na kuchukua nguo zangu na
kutoroka ambapo niliomba lifti kwenye gari la mkaa na kushushwa Ubungo
jijini Dar,” alisimulia mwanamke huyo huku akiapa kutorudi kwa mzee huyo
ambaye hakupatikana kwani hana simu.
Kwa sasa mwanamke huyo amehifadhiwa kwa Mwenyekiti Mtaa wa Shimo la
Udongo, Kurasini kwa mama Felister Komba ambaye baada ya kufika kwake
alimpeleka Kituo cha Polisi cha Kurasini na kufunguliwa faili la taarifa
lenye namba KUR/340/2014.

0 Comments