Kiongozi wa vikosi vya Afrika katika Jamhuri ya Afrika Kati (MISCA),
Jenerali Jean-Marie Michel Mokoko, amemsimamisha kwa muda kamanda wa
kikosi kinachoendesha shughuli zake Boali ambako raia 11 wametoweka
wakati wa operessheni ya MISCA mnamo tarehe 24 Machi. Taarifa ya Umoja
wa Afrika imesema Jenerali Mokoko ameamua kumsitisha kazi kwa muda
kamanda wa kikosi cha Boali na kuwahamisha wanajeshi wote waliokuwepo
Boali wakati wa tukio hilo. Hatua hiyo inaangaliwa kama njia mojawapo ya
kurahisisha uchunguzi unaoendelea. Uchunguzi huo umeanzishwa kufuatia
ripoti ya shirika linalopigania haki za binaadamu la Human Rights Watch
inayosema wanajeshi wa Kongo Brazaville wanaotumikia MISCA wanahusika na
kutoweka raia hao 11 katika mkoa wa Boali, umbali wa kilomita 80
kaskazini magharibi ya mji mkuu, Bangui.
0 Comments