MJAMZITO Agatha Isack (19) amekufa kwa kipigo kutoka kwa mumewe akisaidiwa na mwanamke anayeaminika kuwa hawara yake, akimtuhumu kuwa mvivu wa kulima shambani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari
alithibitisha kifo hicho na kuongeza kuwa mama huyo mjamzito ambaye ni
mkazi wa kijiji cha Manga, Kata ya Kasokola wilayani Mlele alifikwa na
umauti akikimbizwa katika zahanati kijijini hapo kwa matibabu na mumewe
huyo Vitus Mlengo (23).
Akielezea mkasa huo unaodaiwa kutokea juzi saa sita mchana nyumbani
kwa wanandoa hao kijijini humo, Kamanda Kidavashari alisema awali baada
ya kipigo mwanamke huyo alikwenda katika zahanati iliyopo kijijini humo
kwa uchunguzi zaidi na matibabu.
Kabla ya kufika hospitalini alikwenda kwa mama yake mdogo aitwae
Anastazia Charles na kumsimulia jinsi alivyopigwa na mumewe
akishirikiana na Faustina Matheo (31) ambaye anadaiwa kuwa na mahusiano
ya kimapenzi na Mlengo.
“Baada ya kutibiwa Agatha alipitia nyumbani kwa bibi yake kijijini
humo na kumweleza jinsi alivyopigwa na mumewe pia alimfahamisha bibi
yake kuwa mumewe alimuonya asirudi nyumbani bila mboga hivyo bibi yake
huyo alimpatia mboga naye akarejea kwake,“ alibainisha Kamanda
Kidavashari.
Inadaiwa alipofika nyumbani kwa mumewe, Mlengo alimfukuza ndipo
alirudi kwa bibi yake na kulazimika kulala huko hadi asubuhi
alipofuatana na bibi yake ndipo mumewe akampokea .
Kidavashari alifafanua kuwa juzi, saa mbili usiku Agatha alishindwa
kula chakula alichokipika mwenyewe ndipo mumewe alipoona hali yake
imebadilika ndipo alilazimika kuomba msaada wa pikipiki kwa rafiki yake
aitwae Alfred Kasonso na kumkimbiza katika zahanati kijijini humo kwa
matibabu .
Kamanda alithibitisha kuwa mume wa marehemu huyo na Faustina wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.
0 Comments