Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kahama James Lembeli leo ametangaza rasmi kukihama chama cha Mapinduzi na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, huku akitangaza nia ya kuwania Ubunge katika jimbo la Kahama Mjini kupitia Chadema.
Akizungumza na waandishi wa habari jiji Dar-es-salaam, leo Lembeli amesema amechukua uamuzi huo kutokana na kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM, huku uongozi wa chama wilaya ukidai kuwa amekidhalilisha chama kwa madai kuwa amesema maneno ya uongo.
Lembeli amesema uongozi wa CCM wilaya ulikiuka taratibu za chama na kuruhusu baadhi ya wanasiasa kuanza kufanya kampeni za ubunge mapema, huku pia kadi za chama hicho zikitolewa kiholela kwa misingi ya rushwa.
Amesema aliitwa katika kamati ya maadili na kutakiwa kutoa ushahidi wa malalamiko yake ambapo alifanya hivyo na kutaja majina ya wahusika ambao wengine wanatoka ofisi ya CCM wilaya likini viongozi hao walizidi kuwaunga mkono watuhumiwa hao.
Amesema kutokana na hali hiyo ameamua kujiunga na CHADEMA, ambapo ametangaza rasmi nia ya kuwania ubunge katika jimbo la Kahama Mjini, ambapo amesema kama chama hicho kitampa ridhaa hiyo ataendelea kushirikiana na wananchi wa Kahama na Ushetu.
Hata Hivyo Lembeli amewataka wanavikundi vya ujasiriamali na vikundi vya akina Mama kutokata tamaa kwa uamuzi wake huo, kwani ataendelea kuviunga mkono na kuvisaidia bila kujali vya jimbo la Kahama mjini au jimbo jipya la Ushetu.
0 Comments