MALIKIA
wa mipasho nchini, Khadija Kopa ‘Top In Town’, ameponda tuzo za muziki
za Kilimanjaro msimu huu, kwa madai kuna watu hawakustahili kupata, huku
wakiwaacha wale wenye uwezo mkubwa.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam juzi,
Kopa alisema hayasemi hayo kutokana na yeye kutopata tuzo, ila
alishangazwa na tuzo ya mtunzi bora wa nyimbo, aliyopewa Nassib Abdul
‘Diamond’ huku akinyimwa Abelinego Damiani ‘Belle 9’.
Malikia Kopa alisema yeye binafsi pia hajawahi kuona msanii kokote
duniani anapata tuzo saba wakati kuna wenzake wengi, huku akihoji sababu
za Diamond kupata tuzo zote hizo huku muandaaji wake wa muziki akikosa
tuzo hata moja.
“Diamond kapata tuzo zote hizo, lakini ‘producer’ wake hajapata tuzo,
hapo inakuingia akilini? Na hata tuzo ya mtunzi wa taarabu, watu
ukumbini walisema Abuu, lakini akapewa mwingine, hilo ni tatizo
waliangalie tena katika mashindano yajayo,” alisema na kuongeza kuwa
yeye hana kinyongo kukosa tuzo, ila hastaili kuchanganywa na waimbaji
watoto, inatakiwa iwepo tuzo ya wakongwe kama yeye na akina Mwanahawa.
Alisema kila akikaa na kusikiliza nyimbo za Belle 9, huwa anafarijika
mno na kujiuliza kijana huyo maneno ya kuimba anayatoa wapi, lakini
tuzo kanyimwa, inasikitisha.
Aliongeza kuwa kinachomshangaza, mwaka jana wao waliposhinda
walitembelea mikoani kufanya ‘tour’, lakini mwaka huu hayumo kwenye
tuzo, lakini wanamfuata kumtaka aende mikoani.
“Mimi sio mshindi, lakini nafuatwa kutokana na ubora wangu, mwaka
jana tulienda peke yetu mikoani na tukafanya vema, hivyo basi na hawa
waende wakafanye wao kama sisi tulivyofanya mwaka jana, lakini
nimezungumza nao na tukikubaliana nitaenda,” alisema Kopa.
0 Comments