WATU
FULANI HUDHANI kwamba kulala usingizi ni kupoteza wakati. Wao huwa na
shughuli nyingi za kibiashara na kirafiki kila siku, na hulala tu
wanapokuwa wachovu sana. Kwa upande mwingine, wengine hutamani sana
kupata usingizi mtamu lakini hujigeuza-geuza kitandani hadi asubuhi.
Kwa
nini baadhi ya watu hushindwa kulala, hali wengine wanatamani sana kuwa
macho? Je, tuuone usingizi kuwa starehe tu au ni muhimu? Ili kujibu
maswali hayo, ni lazima tufahamu mambo yanayotukia tunapolala.
Mambo Yasiyojulikana Kuhusu Usingizi
Kile kinachomfanya mtu apoteze fahamu na kulala usingizi bado
hakijulikani. Hata hivyo, watafiti wamegundua kwamba usingizi ni
utaratibu tata unaorudiwa na ubongo baada ya kila saa 24.
Tuendeleapo kuzeeka, mazoea yetu ya kulala hubadilika. Mtoto mchanga
hulala kwa vipindi vingi vifupi vyenye jumla ya saa 18 hivi kwa siku.
Kulingana na wataalamu wa usingizi, watu fulani wazima wanahitaji kulala
kwa muda wa saa tatu tu huku wengine wakihitaji muda wa saa kumi.
Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha pia kwamba vijana fulani huona
ugumu wa kuamka asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya utendaji wa mwili.
Yaonekana mwili wa vijana hubadilika wanapobalehe, na ndiyo sababu wao
hutaka kulala usiku sana na kuamka wakiwa wamechelewa. Mazoea hayo ni ya
kawaida nayo huendelea hadi miaka ya katikati na ya mwisho ya ujanani.
Utendaji wa miili yetu huongozwa na kemikali zilizo mwilini na tayari
nyingi zinajulikana. Mojawapo ya kemikali zinazodhaniwa zinasababisha
usingizi ni homoni inayoitwa melatonin.
Homoni
hiyo hutengenezwa kwenye ubongo, na baadhi ya wanasayansi wanaamini
kwamba ndiyo inayopunguza utendaji wa mwili kabla tu ya usingizi. Homoni
hiyo inapotengenezwa, joto la mwili na damu inayoenda kwenye ubongo
hupungua, na pole kwa pole misuli yetu hulegea. Ni nini kinachotukia mtu
anapoanza kulala usingizi?
“Njia Kuu ya Asili Inayoburudisha”
Muda wa saa mbili hivi baada ya kulala usingizi, macho yetu huanza
kusogea-sogea haraka. Jambo hilo limewafanya wanasayansi wagawanye
usingizi katika vipindi viwili: kipindi cha kusogeza macho haraka na
kipindi cha kutosogeza macho.
Kipindi
cha kutosogeza macho kinaweza kugawanywa katika vipindi vingine vinne
vya usingizi mzito zaidi. Vipindi hivyo viwili hubadilishana mtu
anapolala usingizi mzito.
Mara nyingi, mtu huota ndoto wakati wa kipindi cha kusogeza macho. Pia
misuli ya mwili hulegea kabisa, na hivyo mtu huamka akiwa mchangamfu.
Isitoshe, watafiti fulani wanaamini kwamba habari mpya huhifadhiwa
katika kumbukumbu letu la kudumu katika kipindi hicho cha usingizi.
Wakati wa usingizi mzito (kipindi cha 3 na cha 4 cha kutosogeza macho),
shinikizo letu la damu na mpigo wa moyo hupungua zaidi, na hivyo
kupumzisha mzunguko wa damu na kumwepusha mtu na ugonjwa wa moyo. Zaidi
ya hilo, homoni nyingi za ukuzi hutengenezwa wakati wa kipindi cha
kutosogeza macho huku miili ya vijana fulani ikitengeneza homoni za
ukuzi mara 50 zaidi wakati wa usiku kuliko mchana.
Ubongo
wetu huona ukosefu wa usingizi kuwa ukosefu wa chakula. Tunapolala,
mwili wetu hutengeneza homoni inayoitwa leptin, inayojulisha mwili wetu
kwamba tumeshiba.
Tunapokuwa
macho kwa muda mrefu sana, mwili wetu hutengeneza kiasi kidogo cha
leptin, na kutufanya tutamani sana chakula cha wanga. Kwa hiyo, kukosa
usingizi kunaweza kutufanya tule chakula kingi cha wanga, na hivyo
tunenepe kupita kiasi.
Muhimu kwa Afya
Isitoshe, usingizi huwezesha mwili wetu kuharibu kemikali ambazo
inasemekana zinasababisha kansa na kufanya chembe zizeeke. Katika
uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Chicago,
wavulana 11 wenye afya waliruhusiwa kulala kwa muda wa saa nne tu kwa
siku sita.
Baada
ya kipindi hicho, chembe zao zilifanya kazi kama chembe za watu wenye
umri wa miaka 60, na kiwango cha insulini kwenye damu yao kilikuwa kama
kile cha mtu mwenye ugonjwa wa sukari! Kukosa usingizi huathiri pia
utengenezaji wa chembe nyeupe za damu na homoni iitwayo cortisol, jambo
ambalo humfanya mtu apate maambukizo na magonjwa ya damu kwa urahisi.
Bila shaka, usingizi ni muhimu kwa afya ya mwili na ya akili. Kulingana
na mtafiti William Dement, mwanzilishi wa kituo cha kwanza cha
kuchunguza usingizi katika Chuo Kikuu cha Stanford Marekani, “inaonekana
kiwango cha usingizi ambacho mtu hulala ndilo jambo muhimu zaidi ambalo
huamua muda atakaoishi.”
Deborah
Suchecki, mtafiti kwenye kituo cha kuchunguza usingizi huko São Paulo,
Brazili, anasema hivi: “Kama watu wangalijua jinsi kutolala usingizi
kunavyoathiri mwili, hawangalisema kwamba kulala ni kupoteza wakati au
ni uvivu.”.
Lakini je, usingizi hupumzisha mwili nyakati zote? Kwa nini watu wengine
hulala usiku kucha na bado huamka wakiwa wachovu? Makala inayofuata
itakusaidia kutambua baadhi ya matatizo makubwa yanayoletwa na ukosefu
wa usingizi na itaeleza jinsi unavyoweza kupata usingizi wa kutosha.
MATOKEO YA KUKOSA USINGIZI
MATOKEO YA MUDA MFUPI
▪ Kusinzia
▪ Hisia zinazobadilika- badilika
▪ Kusahau mambo kwa muda mfupi
▪ Kushindwa kupanga mambo na kuyatimiza
▪ Kutokuwa makini
MATOKEO YA MUDA MREFU
▪ Kunenepa kupita kiasi
▪ Kuzeeka mapema
▪ Uchovu
▪ Hatari kubwa ya kupatwa na maambukizo, ugonjwa wa sukari, magonjwa ya moyo, na matatizo ya tumbo
▪ Kusahau mambo sana
KULALA KIDOGO MCHANA
Je, umewahi kulemewa na usingizi baada ya chakula cha mchana? Hiyo
haimaanishi kwamba hukulala vyakutosha. Ni kawaida kusinzia wakati wa
mchana kwa sababu joto la mwili hupungua wakati huo.
Kwa
kuongezea, hivi majuzi wanasayansi wamegundua kwamba kuna protini
inayoitwa hypocretin, au orexin,inayotengenezwa na ubongo ambayo
hutusaidia kuwa macho. Kuna uhusiano gani kati ya hypocretin na chakula?
Tunapokula, mwili hutengeneza homoni inayoitwa leptin ambayo hutufanya
tuhisi tumeshiba. Lakini homoni hiyo huzuia utengenezaji wa hypocretin.
Yaani,
kadirileptin inavyokuwa nyingi kwenye ubongo, ndivyo hypocretin
inavyopungua na tunahisi usingizi zaidi. Labda hiyo ndiyo sababu katika
nchi fulani watu hulala kidogo baada ya kula chakula cha mchana.
0 Comments