WATU wanane wamekufa papo hapo, wengine tisa wakijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi baada ya gari aina ya Land Rover, mali ya Halmashauri ya Mji Masasi kupata ajali katika kijiji cha Mtama wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi.
Gari
hilo lenye namba za usajili STL 1615, lilikuwa linatokea Lindi ambako
maofisa wa Halmashauri ya Masasi walikuwa wanashiriki katika Maonesho ya
Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Ngongo,
nje kidogo ya Manispaa ya Lindi.
Kutokea
kwa ajali hiyo kulithibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa
Lindi, Renatha Mzinga aliyesema ilitokea juzi majira ya saa 11.30 jioni
katika kijiji cha Mtama.
Aliwataja
waliokufa kuwa ni Issa Salumu (33), Malik Selemani (24), Juma Ausi
(21), Rajab Khalfan (17), Said Mchora (24) na Fadhili Mchalasi (26)
ambapo watu wawili hadi sasa hawajafahamika majina yao, na amesema
chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi.
Marehemu
wote ni wakazi wa kijiji cha Mtama. Kwa mujibu wa Kamanda Mzinga,
waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni dereva wa gari hilo, Kessy Mwaijande
(40).
Pia
wamo madiwani watano wa Halmashauri ya Mji Masasi ambao ni Habiba
Amlima, Maimuna Chiputa, Exaveria Mhagama, Asha Abbas na Blandina
Nakajumo.
Wengine ni Abraham Mohammed, Shaabani Issa Kitemwe na Ally Adam, wote wakazi wa kijiji cha Mtama.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa majira ya
jioni kwenye eneo hilo la tukio, waliliona gari hilo likiwa kwenye
mwendo kasi, mazingira ambayo yalisababisha dereva wa gari hilo
aliyekuwa akijaribu kukwepa mbuzi waliokuwa barabarani kushindwa
kumiliki gari hilo na hatimaye kuacha njia na kuwagonga watu waliokuwa
pembezoni mwa barabara hiyo, waliokuwa wakifanya biashara ndogo.
Hata
hivyo, mmoja wa mashuhuda hao, Ahmad Mbonde alisema kuwa, kama si
kuwakwepa mbuzi, dereva wa gari hilo asingesababisha ajali.
Kutokana
na tukio hilo, Kamanda Mzinga amewataka madereva kuzingatia sheria za
usalama barabarani ili kunusuru maisha ya watu wanaoendelea kupoteza
maisha na huku wengine wakibaki na ulemavu, mazingira ambayo hupunguza
nguvu kazi ya Taifa
0 Comments