BAADA ya kushikiliwa kwa takriban miezi tisa
kwa kesi ya madawa ya kulevya ‘unga’, hatimaye Video Queen maarufu
Bongo, Jacqueline Fitzpatrick Cliff ‘Jack Patrick’
amehukumiwa kifungo cha miaka 6 jela huku kukiwa na uwezekano wa
kupunguziwa adhabu ikawa ndogo zaidi, Amani linaibumburua habari kamili.
HUKUMU NYEPESI?
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa Jack, modo huyo alihukumiwa Jumatatu
iliyopita (Agosti 11, mwaka huu) kwenye Mahakama ya Macau huko Hong Kong
ambapo hukumu hiyo ilitofautiana na adhabu nyingine za madawa nchini
humo ambazo huwa hukumu yake ni kunyongwa hivyo ya Jack kuonekana
nyepesiii! KWA NINI NYEPESI?
Kikimwaga data, chanzo hicho makini kilidai kwamba, hukumu hiyo ya
Jack ni nyepesi ukilinganisha na hukumu nyingine za madawa ya kulevya
zinazotolewa nchini China ambapo hakimu alitumia muda wa dakika 27 tu
kuisoma.
“Hukumu za madawa ya kulevya zinatofautiana nchini China.
Kuna baadhi ya majimbo kama Beijing huwa wao ikithibitika umebeba madawa
ya kulevya, unanyongwa lakini baadhi ya maeneo unafungwa miaka kadhaa.
Miaka hutofautiana kulingana na sheria walizojiwekea,”
kilifunguka chanzo chetu. HUKUMU YA JACK IPOJE? Ilidaiwa kwamba, kwa
mujibu wa hukumu hiyo aliyohukumiwa mrembo huyo, anaweza kupunguziwa
muda wa kifungo kulingana na nidhamu atakayoionesha gerezani kama
mahakama ilivyoelekeza.
“Anaweza akapunguziwa kifungo kwa sababu hukumu imeeleza wazi
kwamba anaweza kupunguziwa adhabu hiyo kama atatimiza masharti ya
kinidhamu ambayo sheria za China zinamtaka atimize,” kilisema chanzo hicho.
TUJIUNGE NA CHANZO “Amehukumiwa juzi Jumatatu, ametakiwa kwenda jela
miaka sita, nilikuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara lakini juzi hiyo
ndiyo kanitumia taarifa kwamba amehukumiwa na kunieleza kwamba siku hiyo
aliduwaa kwa muda maana hakuamini kama anaweza kuhukumiwa kwani alikaa
muda mrefu bila kujua hatima yake,” kilisema chanzo hicho kilicho karibu
na Jack.
JACK AFURAHIA HUKUMU! Chanzo hicho kilizidi kumwaga data kuwa, baada
ya hukumu hiyo kupitishwa, Jack alifurahia hususan kuwepo kwa kipengele
cha uwezekano wa kupunguziwa kifungo kama atakidhi masharti aliyopewa na
mahakama.
“Baada ya kutafakari kwa kina hukumu yake, Jack anaonekana kuifurahia
kwa sababu anaamini kwake yeye itakuwa ni rahisi kutimiza masharti ya
kuwa mstaarabu kadiri kipengele hicho kilivyomuelekeza,” kilisema
chanzo. NDUGU HAWAJUI LOLOTE? Katika hatua nyingine, chanzo hicho
kilifunguka kuwa ndugu wa Jack waliopo Bongo hawakuwa na taarifa zozote
kuhusiana na hukumu hiyo.
Kilisema kuwa kwa upande wake iliwezekana kupata haraka taarifa hizo
kwani alikuwa akiwasiliana na Jack mara kwa mara kwa njia ya barua.
“Ilikuwa ni rahisi mimi kunipa taarifa hizi haraka kwa sababu nilikuwa
nikiwasiliana naye mara kwa mara, labda sasa hivi kwa kuwa nawapa ninyi
(waandishi wetu) hizi taarifa ndiyo wanaweza na wao kujua
kinachoendelea,” kilisema chanzo hicho.
NDUGU WASAKWA Wakati gazeti hili linakwenda mtamboni, lilifanya
jitihada za kuwatafuta ndugu wa Jack waishio jijini Dar lakini jitihada
hizo hazikuzaa matunda kwani namba zao za simu zilikuwa hazipatikani.
Hata hivyo, rafiki wa karibu wa familia ya Jack ambaye hakutaka jina
liandikwe gazetini alisema wamezipokea habari hizo kwa furaha kwani
kulikuwa na hofu kubwa kuwa huenda ndugu yao akanyongwa.
“Ndugu, jamaa na marafiki wa karibu na Jack wameipokea hukumu hiyo
kwa furaha maana walikuwa wakihofia adhabu ya kunyongwa ambayo inatolewa
zaidi nchini China,” alisema rafiki huyo wa familia. JUX NAYE Ili
kuzidi kujiridhisha zaidi, mapaparazi wetu walimtafuta rafiki wa karibu
wa Jack ambaye alikuwa akitajwa kuwa mpenzi wake, Juma Khalid ‘Jux
Vuitton’ lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
TUJIKUMBUSHE Jack alikamatwa Desemba 19, mwaka jana akiwa amebeba
madawa ya kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa kilo 1.1 katika Uwanja
wa Ndege wa Macau akitokea jijini Bangkok nchini Thailand kuelekea
Guangzhou, Mji Mkuu wa Jimbo la Guangdong Kusini mwa China.
0 Comments