STAA wa muziki wa Bongo fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’,
amesema licha ya kutafuta video zenye kiwango, pia dharau na mapozi ya
watayarishaji wengi wa Tanzania yamechangia kuacha kutengeneza kazi zake
nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda nchini Canada,
Diamond alisema mtayarishaji unalipa hela kwanza ndio anakufanyia kazi
zako, lakini watayarishaji wa hapa nchini ukishawalipa, kinachofuata ni
usumbufu katika kukamilisha kazi.
“Siwezi kumlipa mtayarishaji milioni 40 alafu aniletee dharau, hajui
hiyo hela nimeipata vipi. Wengi wao wamekuwa na dharau kama vile
wanafanya kazi bure, ndiyo maana nimekuwa nikifanya kazi nje ya nchi,”
alisema Diamond.
Akifafanua zaidi, alisema unaweza ukamweleza mtayarishaji mfike studio saa 12 asubuhi, lakini atakuja saa nne.
“Kwangu hizo ni dharau, kama unaweza kuachana naye, yaani ukishamlipa hela ndiyo kabisa ni mapozi tu,” alisisitiza.
Diamond, mmoja wa nyota mahiri wa muziki wa Bongo fleva nchini, kwa
sasa anatamba na ngoma yake ya ‘Mdogo mdogo’ aliyoifanyia nchini Afrika
Kusini chini ya mtayarishaji mahiri, Godfather.
0 Comments