Mbunge wa
Vunjo, Augustine Mrema (TLP) amedai kitendo cha yeye kubaki kwenye
Bunge Maalumu la Katiba kumetumiwa vibaya na wahasimu wake wa kisiasa
jimboni kwake.
“Ukawa
na ubunge wa Vunjo vimegeuka propaganda chafu dhidi yangu. Wamediriki
kuwaambia wananchi wangu kuwa nimeahidi kuwaachia jimbo langu,” alisema.
Mrema
ambaye pia ni mwenyekiti wa taifa wa TLP, alitoa kauli hiyo jana jimboni
kwake katika mkutano na waandishi wa habari aliouitisha kuelezea kwa
nini hakuwaunga mkono Ukawa.
Mrema
alisema malengo ya Ukawa siyo katiba bali Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na
ndiyo maana tangu waliposusia Bunge agenda yao imebadilika na kuwa
muungano wa kuelekea uchaguzi 2015.
“Mimi nimeamua kubaki bungeni kwa ajili ya masilahi mapana ya wananchi
wa jimbo langu la Vunjo na Watanzania kwa jumla. Sitishwi na Ukawa na
nitatetea kiti changu 2015,” alisisitiza.
Mrema
alitumia mkutano huo kumshambulia mbunge wa kuteuliwa na Rais, ambaye ni
James Mbatia kutokana na uamuzi wake wa kutangaza nia ya kuwania ubunge
wa Jimbo hilo mwakani. Kwa mujibu wa Mrema, ndiye Mtanzania pekee
mwenye sifa na aliweza kugombea ubunge katika majimbo matatu tofauti na
kushinda.
“Mimi ni Mtanzania pekee ambaye nimewahi kuwa mbunge wa majimbo matatu
tofauti ya Moshi Vijijini, Temeke na Vunjo. Sifa hizo hazipo kwa
wengine,” alisema.
0 Comments