Na.Joseph Ngilisho,Arusha
Ukistajabu ya Mussa, utapata ya Firauni,mtoto wa kike mwenye umri wa
mwaka mmoja na nusu (jina linahifadhiwa),mkazi wa Sokoni One jijini
hapa, amebakwa na kunajisiwa na mwanamme mwenye umri wa miaka 30.
Mtuhumiwa ametajwa kwa jina la Rajabu Mkoba, mkazi wa eneo hilo.
Ilidaiwa mtuhumiwa alimbaka mtoto huyo kwa zaidi ya saa 9 baada ya
kumchukua kwa mtu aliepewa kumtunza.
Tukio hilo lilitokea Agosti 3 mwaka huu huku mama mzazi wa mtoto huyo,
Mwitango Yambazi Mtalu (27), akishindwa kutoa taarifa polisi baada ya
kuahidiwa shilingi 100,000.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mama wa mtoto huyo, alisema
siku ya Jumapili majira ya asubuhi alimkabidhi mtoto wake kwa jirani
yake aliyemtaja kwa jina la Mustafa Kabananga, ili apate nafasi ya
kushiriki mkutano wa kikundi chake.
Alisema baada ya kurudi jioni majira ya saa mbili usiku alikwenda kwa
jirani yake huyo kwa lengo la kumchukua mtoto wake lakini aliarifiwa
mtoto wake alichukuliwa na kijana aliyemtaja kwa jina la Rajabu ambaye
anafahamika eneo hilo.
Alisema aliamua kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa ambaye anaishi na wazazi
wake, hata hivyo hakufanikiwa kumkuta wala mtoto wake na kurejea
nyumbani huku akiendelea na jitihada za kumtafuta.
Alisema aliamua kwenda kituo cha polisi Unga Limited kumuulizia
akiongozana na balozi wa nyumba kumi.
Hata hivyo, polisi walimtaka arudi nyumbani hadi asubuhi arejee kituloni
kwa ajili ya taratibu nyengine.
Alisema wakati akirejea nyumbani majira ya saa 9 usiku alimkuta mama
mzazi wa mtuhumiwa aliyetambukika kwa jina la mama Mkoba akiwa na mtoto
wake akimrejesha huku mtuhumiwa akiwa hayupo.
Baada ya kukabidhiwa aliamua kumchunguza vizuri ndipo alipokuta sehemu
za siri za mtoto wake zimevimba kupita kiasi huku damu ikitoka mara kwa
mara.
Aliamua kumweleza mama wa mtuhumniwa jinsi mtoto wake alivyoharibiwa,
ambapo mama huyo alimsihi asitoe taarifa popote na kwamba atampatia
shilingi 100,000 na kumpeleka mtoto huyo hospitali.
Hata hivyo, mama wa mtuhumiwa baada ya kukabidhiwa mtoto huyo,
hakumpeleka hospitali yeyote badala yake alikuwa akimtibu kwa kutumia
miti shamba.
Lakini baadhi ya majirani walikerwa na kitendo cha mama wa mtoto
kunyamazia unyama huo ndipo walipomvamia kwa maneno makali na kumtaka
alifikishe suala hilo kwenye vyombo vya sheria.
Kufuatia kelele za majirani ndipo alipokubali kwenda kituo cha polisi
Unga Ltd ambapo polisi walifika nyumbani kwa mama wa mtuhumiwa na
kumchukua mtoto huyo kumpeka hospitali ya Mount Meru.
Mama wa mtoto huyo na wa mtuhumiwa wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano
huku mtuhumiwa akiendelea kusakwa.
You might also like:
0 Comments