JESHI la Polisi nchini limesema hakuna
mtu yeyote anayehojiwa au kushikiliwa na jeshi hilo akihusishwa na madai
ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kuwepo
kwa njama za kutaka kumuawa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad
Slaa.
Ijumaa iliyopita, madiwani wawili wa
chama hicho kutoka mkoani Shinyanga, waliorejea tena na Chadema baada ya
mapema mwaka huu kukihama na kuingia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
waliibua tuhuma nzito dhidi ya baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM
kwamba walikuwa na mpango wa kuidungua helikopta aliyokuwa akiitumia Dk.
Slaa na viongozi wengine wa juu wa chama hicho. Madiwani hao ni Peter
Sebastian ‘Obama’ wa Kata ya Ngokolo na Martine Mfuko wa Kata ya
Msekelo, Shinyanga.
Akizungumza jana na Raia Tanzania,
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema mbali na
kuzisikia na kuzisoma tuhuma hizo kwenye vyombo vya habari, jeshi hilo
halijapokea taarifa au malalamiko kutoka kwa viongozi wa Chadema Mkoa wa
Shinyanga wala Makao Makuu Dar es Salaam kuhusu suala hilo zito.
Alisema kama Jeshi la Polisi lingepata
taarifa hizo, ni wazi hatua stahiki zingechukuliwa ikiwa ni pamoja na
kufanyika kwa upelelezi dhidi ya yeyote anayehusika au kuhusishwa na
suala hilo.
“Hatuwezi kuchukua hatua yoyote kwa sasa
kwani viongozi hao (madiwani wa Chadema) hawajatoa taarifa. Inawezekana
kuwa hizo ni siasa tu,” alisema Mangu.
“Kazi zetu zinafanyika kwa taratibu
zake, na katika hili, hatuna kitu chochote cha kukifanyia kazi kwani
hakuna taarifa iliyoripotiwa kwetu. Ingekuwa ni busara kwa viongozi hao
kutoa taarifa juu ya njama za kudunguliwa helikopta ya Chadema. Sasa
kukaa kwao kimya, jeshi litaanzia wapi uchunguzi?” alisema na kuhoji
IGP, huku akisistiza kuwa taarifa hizo ni michezo ya kisiasa tu.
0 Comments