MBUNGE
wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amesema hatagombea ubunge
kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwa kuwa amechoshwa na kauli
za vitisho na kejeli dhidi yake, zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa
juu wa chama hicho.
Amesema
hayo jana kwa nyakati tofauti, wakati akizungumza na wazee wa Mji wa
Maswa na Malampaka wilayani humo, alipokuwa akijibu swali lao kuhusu
hatima yake ya kisiasa ndani ya Chadema, baada ya chama hicho kutishia
kumfukuza.
Alipoulizwa
na wazee ni chama kipi atagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao,
alisema wakati ukifika atasema kwani kwa sasa bado anatimiza wajibu wake
wa kutetea wapiga kura wake ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji na
yuko tayari kufukuzwa ndani ya Chadema kwa kuwatetea wao.
Alisema
kuwa aliingia katika chama hicho kwa hiari yake baada ya kukataa
dhuluma alizodai kufanyiwa na CCM na kudhani ndani ya Chadema kuna
demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini alichokikuta ni tofauti kwani
kila siku amekuwa akipata misukosuko kutoka ndani ya chama hicho.
"Mie
niliingia Chadema kwa hiari yangu baada ya kuona dhuluma zilizokuwa
ndani ya CCM, chama kilichonilea kisiasa, nikaona heri niende Chadema
ambako nilidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini
nilichokikuta humo ni tofauti kwani kila siku wazee wangu mnasikia
napata misukosuko isiyo na maana," alisema.
Alisema
pamoja na misukosuko hiyo, amekuwa kimya muda mrefu kiasi kwamba kuna
wakati vijana ndani ya chama hicho walimtukana matusi, wakatoa maneno
mbalimbali ya kumdhalilisha kwa kumwita ‘Msaliti’ na ‘Pandikizi wa CCM’,
huku viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho, wakikaa kimya bila
kuchukua hatua.
"Pamoja
na shutuma zote zinazotolewa juu yangu na kupachikwa majina mbalimbali
kuwa mie ni ‘Msaliti’ mara ni ‘Pandikizi la CCM’, lakini hata siku moja
sijawahi kuitwa katika Kamati Kuu ya Chadema na kuhojiwa.
“Nimekuwa
nikitukanwa hadharani na vijana wa Chadema mbele ya viongozi wa juu wa
chama, hawachukui hatua… mie mtu mzima hapo natafsiri kuwa wametumwa na
viongozi hao ili kunifanyia fitna hizo," alisema.
Akizungumzia
tuhuma zilizotolewa juu yake za kukiuka msimamo wa kutohudhuria vikao
vya Bunge Maalumu la Katiba, uliowekwa kwa wajumbe wa Bunge hilo kutoka
kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema tuhuma hizo hazina
msingi wowote kwani hajahudhuria kikao hicho wala hakuchukua posho.
Alisema
alifika mjini Dodoma akitokea Dar es Salaam akiwa njiani kwenda katika
Jimbo lake la Maswa Magharibi na alipita bungeni kufuatilia fedha za
matibabu kutokana na kusumbuliwa na mguu.
Akiwa
bungeni Shibuda alisema alijaza fomu za matibabu kwa kuwa wabunge
wanatibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha uhai
wa ubunge wao.
"Mie
ni kweli nilipita Dodoma nikitokea Dar es Salaam kuja huku jimboni na
nilifika Ofisi za Bunge ili nipatiwe fedha za matibabu kwani nasumbuliwa
na mguu na siye tunatibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa
kipindi chote cha ubunge sasa kosa langu la kuitwa msaliti hapa ni lipi?
“Hata
hiyo posho wanayodai nimeichukua iko wapi? Labda wameweka katika
akaunti ila mie nasisitiza sijachukua posho wala kuhudhuria kikao
hicho," alisema.
Alisisitiza
kuwa tangu habari hizo zianze kuandikwa na kutangazwa katika vyombo vya
habari, hajawahi kuulizwa na kiongozi yeyote wa Chadema, isipokuwa
amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, kutishia
kumfukuza ndani ya chama kwa usaliti.
"Uongozi
ni kutanguliza hekima na busara katika kufikia uamuzi, uongozi si
Magereza na hata Magereza wafungwa wana haki zao, Tundu Lissu amekuwa
nani katika nchi hii… anaongea kama kasuku hafanyi utafiti anakurupuka
na kuongea na kutoa matamko? Mie nitamtaka athibitishe tuhuma hizo
anazozitoa dhidi yangu. Nasema Chadema si baba wala mama yangu," alisema.
Alisisitiza
kuwa amechoka kusikia hukumu dhidi yake kila siku kupitia vyombo vya
habari kutoka kwa viongozi wake wa Chadema, huku akitoa mfano kuwa
alipounga mkono nyongeza ya posho ya Bunge, aliitwa ‘Msaliti’, lakini
leo wabunge wote wakiwemo wa Chadema waliogomea wanachukua posho hiyo.
"Wazee
wangu niliposema bungeni posho iongezwe, niliitwa mie ‘Msaliti’ na
wabunge wa Chadema lakini leo kila mmoja muulizeni hata huyu Kasulumbayi
(Sylvester, Mbunge wa Maswa Mashariki, Chadema), ambaye tunaye hapa
kwenye kikao kama hachukui posho hizo.
“Hata
huyo Tundu Lissu anayeongea sana anachukua, hata Mbowe (Freeman,
Mwenyekiti wa Chadema) alikataa gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, lile la Serikali lakini hadi leo analitumia… mbona
yeye haitwi ‘Msaliti’?” Alihoji Shibuda.
Akizungumzia
uhusika wake katika kundi la Ukawa, Shibuda alisema kuwa yeye si sehemu
ya kundi hilo na wala hajawahi kuelimishwa kuhusu kundi hilo, bali
anakumbuka kuwa kupitia viongozi wa juu wa vyama vya Chadema, CUF na
NCCR –Mageuzi, walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wa vyama hivyo
watoke bungeni na wasishiriki vikao hivyo.
"Muislamu
hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo saba za Uislamu na pia huwezi
kuwa Shekhe bila kupitia Madrasa na hata katika Ukristo, huwezi kuutetea
Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho… na mie siwezi kuwa
Ukawa wakati sijaelimishwa kuhusu kundi hilo,” alisema.
Lissu
Lissu alipopigiwa simu ili atoe ufafanuzi, alisema taarifa kwamba Shibuda amepokea posho katika Bunge Maalum la Katiba, alizipata kwa waandishi wa habari. Alipoulizwa kama alijaribu kuthibitisha taarifa hizo, alisema taarifa hizo zimeelezwa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad.
Lissu alipopigiwa simu ili atoe ufafanuzi, alisema taarifa kwamba Shibuda amepokea posho katika Bunge Maalum la Katiba, alizipata kwa waandishi wa habari. Alipoulizwa kama alijaribu kuthibitisha taarifa hizo, alisema taarifa hizo zimeelezwa kwa waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad.
Lissu
alisisitiza kwamba Shibuda alisaini posho mara moja, na ndio maana
Katibu wa Bunge hilo, aliwaambia waandishi wa habari na yeye kupata
taarifa hizo kupitia magazeti.
Kuhusu
Shibuda kutogombea Ubunge kupitia Chadema, alisema angemshangaa kama
asingetoa ujumbe huo, kwani amekuwa akienda kinyume na msimamo wa
wenziwe tangu siku ya kwanza ya kuanza kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
“Shibuda
kwenda kinyume na wenzake hajaanza leo, ameanza siku ya kwanza tu
wakati Rais Jakaya Kikwete alipozindua Bunge na hajabadilika, kwa hiyo
kutamka msimamo wake ni sawasawa tu,” alisema Lissu.
Alisema
Shibuda anajua mambo yake bungeni hivyo wangeshangaa kama bado angekuwa
na nia ya kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho.
0 Comments