Advertisement

Responsive Advertisement

UKAWA WATANGAZA RASMI KUTORUDI BUNGENI WALA KUSHIRIKI VIKAO VYA MARIDHIANO


MCHAKATO wa katiba mpya umefikia hatua ngumu zaidi kuliko ilivyotarajiwa baada ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutangaza rasmi kutoshiriki vikao vya maridhiano na mikutano ya Bunge Maalum.
 
Kwa takribani miezi miwili sasa kulikuwa na jitihada za kuwashawishi wajumbe hao kurejea bungeni baada ya kususia vikao kwa madai ya kuchoshwa na lugha za ubaguzi, matusi, kejeli na kusiginwa kwa rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Msimamo huo wa UKAWA sasa unaonyesha dhahiri huenda mchakato wa katiba ukakwama licha ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta kutangaza litaanza vikao vyake keshokutwa.

Kukwama kwa mchakato huo kunatokana na ukweli kuwa ili vifungu vya rasimu vipitishwe ndani ya Bunge, vitahitaji theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo kutoka Zanzibar.

Inasadikika kuwa bila ya ushiriki wa wajumbe wa CUF kutoka Zanzibar waliomo kwenye UKAWA, theluthi mbili haitopatikana wakati wa kupiga kura.

Kutokana na jambo hilo, zipo taarifa baadhi ya vigogo wa CCM na serikali wanadaiwa kushiriki kwenye vitendo vya kuwarubuni, ikiwemo kuwapa fedha wajumbe wa CUF walio UKAWA wakiuke msimamo wa kundi lao na waingie bungeni.

UKAWA wanena
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, viongozi na wajumbe wa UKAWA, walisema hawataendelea kushiriki mazungumzo na CCM wala kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum.

Wajumbe hao walisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kutafakari na kuona kuwa tiba ya kuzaa katiba haijapatikana baada ya mazungumzo ya maridhiano ya kikao cha nne kilichoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wenyeviti wenza wa UKAWA, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alisema mazungumzo yaliyoratibiwa na Jaji Mutungi hayana faida kutokana na CCM kuendelea kudai matakwa yao na si muafaka.

Mbowe alisema ushiriki wao katika mazungumzo ya maridhiano walitarajia mabadiliko ya uendeshaji wa Bunge Maalum kwani rasimu inabeba taswira ya nini Watanzania wanataka katika katiba.

Alisema UKAWA ilitaka kuona Bunge Maalum linatekeleza wajibu wake kisheria katika kujadili, kuboresha na kupitisha rasimu ya katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na maoni ya wananchi walio wengi na si kuibomoa, kuibatilisha na kuifuta.

Alisema kuwa sura ya 83 inatambua rasmi rasimu ambayo inabeba maoni ya Watanzania, taasisi na utafiti wa kina ambazo sura zote zinaeleza serikali tatu.

Alieleza kuwa UKAWA inataka misingi iliyowekwa iheshimiwe na sio kubomoa kama ambavyo kanuni zilizowekwa na CCM zinavyoruhusu kuibomoa rasimu hiyo ili wapate kile wanachokihitaji.

Alisema kuwa CCM inatumia jeuri waliyonayo kutokana na kuwa na wabunge wengi walioongezwa kwa hila kupitia baadhi ya wajumbe 201.

Akizungumzia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, Mbowe alisema kuwa udhaifu aliouonyesha katika hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba ameurudia tena Julai 31, 2014 siku moja kabla ya kikao cha nne cha mazungumzo ya UKAWA na CCM.

Alisema kuwa pamoja na kauli za kuvuruga Bunge, Kikwete ndie ameukwamisha mchakato huo.

“Kikwete ameendelea kupotosha matumizi ya kanuni ya 33 ibara ya nane (i) ya kanuni za Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Bunge hilo na kukwepa kuzungumzia marekebisho yaliyofanyika Aprili 25, 2014 baada ya wajumbe wa UKAWA kutoka, ambapo mabadiliko hayo mapya yameingiza kanuni mpya ya 32(6) inayoruhusu Bunge Maalum kupendekeza sura mpya,” alisema.

Alisema kuwa marekebisho hayo yalilenga kupenyeza sura za rasimu ya CCM ya serikali mbili na sura nyingine zilizo kinyume na maoni ya wananchi juu ya Katiba ya Shirikisho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbowe, alisema msimamo potofu wa Kikwete ndio umekuwa msimamo wa wajumbe wa CCM na kukwamisha maridhiano ambayo yangewezesha muafaka wa kunusuru mchakato huo.

Alisema kuwa kutokana na kutorejea katika Bunge la Katiba, wameamua kuanza mazungumzo miongoni mwa viongozi na wajumbe wa UKAWA na wataeleza uamuzi mbadala utakaofanyika ili kuwezesha kupatikana kwa katiba ya wananchi.

Post a Comment

0 Comments