WAFANYABIASHARA tisa wakazi wa Kijiji cha Mpasa wilayani Nkasi
mkoani Rukwa, wanahofiwa kufariki baada ya boti waliyokuwa wakisafiria
kwenda nchini Zambia kuzama kwenye eneo la Kipwa.
Watu hao walikuwa wakienda Zambia kuuza samaki wabichi ambapo walifikwa na mkasa huo katika Wilaya ya Kalambo.
Taarifa iliyopatikana jana na kuthibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Stella Manyanya, ilisema Meneja wa Usimamizi wa Mamlaka ya Usafiri wa
Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Rukwa, David Chiragg ameagizwa
kufuatilia tukio hilo.
Manyanya alibainisha kuwa Chiragg, ameagizwa kufuatilia tukio hilo ikiwemo pia kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kasanga, Wilaya ya Kalambo mkoani humo,
Francis Simfukwe, alikiri kutokea kwa ajili hiyo na kuwataja
waliopoteza maisha kuwa ni Mathias Ulaya (20), Mwambe Ntapantapa (21),
Godfrey Kazumba (24).
Wengine ni Venas Alberto (35), Kashindi Tantika (25), Linus
Maliyatabu (38), Audifas Milele (43), Shabani Kasokota (33) na Fadhili
Nkambi (30).
Alisema wafanyabiasahara hao waliondoka juzi jioni katika Kijiji cha
Mpasa kuelekea Mpulungu walikokwenda kuuza samaki wabichi.
Alibainisha kuwa watu hao walipofika katika Kijiji cha Kipwa, boti
yao ilipigwa na dhoruba lililosababishwa na upepo mkali ulioambatana na
mawimbi makubwa yaliyopindua boti hiyo na baadae ilizama.
Simfukwe, alisema kutokana na tukio hilo kutokea nyakati za usiku,
jitihada za kuwaokoa wahusika zilikuwa ngumu kwakuwa wavuvi na waokoaji
wengine walishindwa kuona vizuri.
Alibainisha kuwa baada ya kucha zoezi hilo liliendelea bila
mafanikio kwakuwa hadi sasa hakuna mwili uliopatikana isipokuwa
kilichoonekana ni masanduku manne ya samaki waliyokuwa wameyabeba.
0 Comments