WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira,
amewapongeza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa kuamua kurudi bungeni ili kuendelea na
mijadala ya Rasimu.
Alisema
wajumbe hao hawapaswi kubezwa bali wanastahili pongezi kwa kutambua
umuhimu wa kutengeneza Katiba kwa maslahi ya nchi na Watanzania kwa
ujumla.
Bw.
Wassira aliyasema hayo juzi wakati akijibu maswali ya waandishi wa
habari wakati akitembelea Mabanda ya Maonesho ya Wakulima na Wafugaji
maarufu kama Nanenane, katika Viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.
"Kilichofanywa
na baadhi ya wajumbe wanounda UKAWA si dhambi bali ni wazalendo
halisi... sioni sababu ya wajumbe hawa kuonekana wasaliti kwani Katiba
tunayoitengeneza si ya chama cha siasa bali ya Watanzania wote," alisema.
Akizungumzia
kamati yake namba sita katika Bunge hilo, alisema kesho wataendelea
kujadili sura ya nne ambapo hadi sasa, wamejadili sura tatu ikiwemo
inayohusu sera za Taifa ambazo ndio msingi wa kutengeneza sera na sheria
kwa ajili ya kusimamia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya
wananchi.
"Sura
ya tatu, inazungumzia maadili na miiko ya viongozi, kama unavyojua,
kumekuwepo na manung'uniko juu ya ubadhirifu, rushwa na kumomonyoka kwa
maadili nchini...baadhi ya watu wanafikiri wakipewa kazi na Serikali,
wanajipanga jinsi ya kuiba badala ya kujituma kazini ili aweze
kuzalisha," alisema.
Aliongeza
kuwa, wajumbe wa kamati yake wameweka vifungu katika rasimu ambavyo
vitakuwa vinaielekeza Serikali jinsi ya kuchukua hatua na namna ya
kuweka vyombo ambavyo vitasimamia maadili pamoja na miiko ya uongozi.
0 Comments