KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod
Slaa, amesema hajawahi kupokea barua yoyote kutoka kwa Msajili wa Vyama
vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, inayowataka waitishe mkutano wa Kamati
Kuu ili kufanya marekebisho ya Katiba yao.
Wakati
Dk. Slaa anatoa kauli hiyo, Julai, mwaka huu, Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika, alizungumza na vyombo vya
habari kuwa Agosti, 2006 walifanya marekebisho makubwa ya Katiba ikiwamo
kifungu kilichokuwa kinaweka ukomo wa uongozi.
Juzi,
Jaji Mutungi alisema kuwa kinachotokea sasa ndani ya chama hicho ni
matokeo ya kupuuzwa ushauri wake wa kukitaka kifanye marekebisho ya
Katiba yake.
Kauli
za viongozi hao zilitokana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe
kuwekewa pingamizi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Tabora, Kansa
Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti taifa, akidai
chama chake kimekiuka Katiba na maagizo ya msajili.
Barua
ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema ya
Januari 15, mwaka huu, ilitaka chama hicho kuitisha mkutano rasmi na
halali kwa mujibu wa Katiba yao.
“Chama
chenu kiitishe mkutano (forum) rasmi na halali kwa mujibu wa Katiba
yenu, kisha mlifanyie upya tafakari stahiki suala linalohusu marekebisho
ya ibara 6.3.2(c) kwa kuzingatia taratibu na hatua zinazopaswa ili
kuwezesha kuwasilishwa kwa ibara hiyo katika Mkutano Mkuu, kwa lengo la
kupitishwa rasmi na mkutano huo ambao ndio wenye mamlaka halali kwa
mujibu wa Katiba ya chama chenu, ili kuwezesha kutumika kihalali,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Jana, Dk. Slaa alisema hakuna barua yoyote ndani ya ofisi yake ambayo imetoka kwa msajili huyo.
“Sijawahi
kupokea barua ya Jaji Mutungi na wala hakuna barua ya aina hiyo ofisini
kwake inayoitaka ofisi yangu kuitisha mkutano wa Kamati Kuu ili kufanya
marekebisho ya Katiba ya chama,” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia
rufaa ya Mbarouk, Dk. Slaa alieleza kushangazwa kwa kitendo cha
kupelekwa kwenye magazeti badala ya kufika kwanza ofisini kwake.
“Kwanza
siwezi kuzungumzia rufaa ya Mbarouk kwa sababu kuna taratibu zake…
lakini kilichonishangaza ni kitendo cha rufaa kupitia kwanza kwenye
magazeti badala ya kuletwa kwanza ofisini,” alisema.
Alipotakiwa
kuzungumzia kauli ya msajili kuwa walipuuza ushauri wake, alisema hata
habari iliyokuwa imeandikwa haikuwa ya kweli bali jaji huyo alilishwa
maneno ambayo hayakusema.
“Bora
hata umejileta mwenyewe… nimetoka kuzungumza na Jaji Mutungi amesema
maneno yaliyoandikwa katika gazeti lenu hayakuwa yake kabisa.
“Ninajua kwanini mnayaandika na malengo yenu nayajua sasa kama mnafanya propaganda tumieni akili.
“Sasa
kaandike hivyo hivyo na usipoandika hayo niliyokueleza ni wazi gazeti
lenu litakuwa na nia mbaya na Chadema… ukiwa na swali jingine wewe
niulize tu,” alisema Dk. Slaa.
Mwandishi
alipomtafuta Jaji Mutungi ili kujua kama ni kweli amemweleza Dk. Slaa
kuwa hakuyasema maneno hayo, alisema hawezi kuzungumza kwenye simu na
badala yake atafutwe leo.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania