Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga |
OPERESHENI ya kukamata madereva
wanaofanya makosa ya barabarani, inayoendana na utozaji wa faini nchini,
imeliingizia Jeshi la Polisi mabilioni ya shilingi. Akizungumza naBongo na matukio juzi, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani,
Mohamed Mpinga, alisema mapato yatokanayo na makosa hayo yaliyokusanywa
kwa miezi sita mwaka huu, yamezidi makusanyo yote yaliyofanyika mwaka
jana.
“Idadi ya makosa yaliyokamatwa mwaka huu
ni mengi, tofauti na mwaka jana. Alisema mwaka huu magari mengi
yamekamatwa. “Hii ina maana kwamba kuna watu walikuwa wanafanya makosa,
lakini hawakamatwi, sasa wanakamatwa, ndio maana wanalalamika, na ni kwa
makosa makubwa tu,” alisema Mpinga.
Alisema takwimu zinaonesha mwaka jana
makosa yaliyokamatwa yalitozwa faini ya Sh bilioni 16, wakati mwaka huu
kuanzia Januari mpaka Juni, yamekamatwa makosa yenye faini ya karibu Sh
bilioni 19.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya
askari wa usalama barabarani wa mkoa wa Dar es Salaam, walidai kuwa
wamepewa malengo ya kukusanya kati ya Sh milioni tano hadi milioni 15
kwa mwezi kwa kila askari mmoja, kutokana na makosa ya barabarani.
Gazeti hili lilifanya mahojiano na zaidi
ya trafiki 10, ambao baadhi walikiri kupewa malengo hayo na wakuu wao
wa kazi, huku baadhi ya madereva wakidai kuelezwa malengo hayo na
matrafiki.
Hata hivyo, taarifa hizo zinatofautiana,
kwani trafiki wengine walidai wameambiwa wafikishe Sh milioni tano na
wengine wakidai 15 na sababu wanazotaja za malengo hayo ni kuongeza
mapato ya Serikali na kusaidia Bajeti Kuu.
“Sisi tumeambiwa lazima tufikishe Sh
milioni 15 kwa mwezi na mabosi wetu wamekuwa wakali sana…wanatuambia
wazi tuache rushwa tupeleke fedha serikalini,” alisema trafiki mmoja
ambaye hakutaka kuandikwa jina gazetini.
Hata hivyo, Kamanda Mpinga alisema madai
kwamba matrafiki wamepewa malengo ya makusanyo, si ya kweli, ila kuna
maelekezo yaliyotolewa kwa askari wakamate makosa mengi iwezekanavyo.
“Sio kweli kwamba tumewapa lengo la
kukusanya fedha kwa mwezi, mikakati ni kwamba askari wakamate makosa
mengi kadiri inavyowezekana na tumewaambia makosa ya kukamata ni yale
hatarishi, wanaodai kupewa kiwango cha fedha za kukusanya ni wavivu wa
kazi,” alisema Kamanda Mpinga.
Makosa hatarishi Kamanda Mpinga alitaja
aina ya makosa ambayo dereva akikutwa nayo anapaswa kukamatwa na kulipa
faini kuwa ni yale yanayoweza kusababisha ajali mbaya za barabarani.
Mfano wa makosa hayo ni mwendo kasi
usiozingatia alama za barabarani, ulevi, kupita taa nyekundu, kupita
mistari ya pundamilia, wanaotanua na wanaopita gari jingine sehemu
isiyoruhusiwa.
Alisema makosa hayo, hayatasamehewa kwa sababu yanaweza kusababisha ajali na watu wakapoteza maisha au kujeruhiwa.
Makosa ya elimu Kamanda Mpinga alisema
kuna makosa ambayo dereva anapaswa kukamatwa na kuelimishwa tu na si
kulipishwa faini, ikiwemo kutofunga mkanda au kutoandika jina katika
ubavu wa gari, kwa magari ambayo yanatakiwa kufanya hivyo.
Alifafanua kuwa katika makosa hayo ya
kuelimishwa, askari anatamuandikia dereva faini ikiwa ameelimishwa zaidi
ya mara mbili katika siku tofauti, lakini amerudia kosa hilo hilo.
Kamanda Mpinga alisema askari wanaodai
kupewa lengo la makusanyo ya fedha na wanaokamata madereva na
kulazimisha makosa ni wavivu, wanajaribu kufikia wenzao wanaofanya kazi,
ili waonekane na wao ni wachapa kazi.
Aliwataka askari wa usalama barabarani,
kuacha kuandikia faini makosa ambayo dereva anapaswa kuelimishwa, kama
rangi ya gari iliyoko kwenye kadi kutofautiana na iliyoko kwenye gari au
kutofunga mkanda, badala yake wajikite kukamata makosa makubwa.
“Hao askari wanaoandikia makosa madogo
madogo na kulazimisha makosa ni wavivu tu…ndio hao wanaochukua rushwa
kwa sababu haiwezekani wenzake kwenye kituo kimoja wakamate makosa zaidi
ya hamsini, yeye akamate makosa mawili, hawa ndiyo wala rushwa
hawatufai kabisa,” alisema.
Alifafanua kuwa kila mwezi askari
wanapimwa utendaji kazi wao, na vipimo ni pamoja na kasi ya kukamata
makosa ambayo ikikutwa ni ndogo, inaashiria kwamba askari ni mla rushwa
na hafanyi kazi yake kwa uaminifu.
Madereva walalamika Baadhi ya madereva
waliozungumza na gazeti hili, walidai kuwa wamekuwa wakikamatwa ovyo na
matrafiki na kutakiwa kulipa faini bila kupewa muda wa kujieleza. Mmoja
wa madereva hao, Said Hokororo, alidai kulazimishiwa makosa ili walipe
faini ya Sh 30,000.
“Kuna siku kulikuwa na trafiki mataa ya
Tazara (Dar es Salaam)… alikuwa akiita magari kutoka Buguruni, ghafla
akaondoka na magari yakaendelea kwenda, akatokea mwingine kwa mbele na
kusimamisha magari zaidi ya matano yaliyopita na kuyaandikia faini
wakati hatukujua kama trafiki aliyekuwa akiongoza alishaondoka,” alidai
Hokororo.
Kwa mujibu wa madai ya Hokororo, trafiki
huyo alipoulizwa sababu ya kuwakamata, alisema aliyekuwa akiongoza
magari amechoka, amekwenda kunywa chai hivyo madereva walipaswa kusimama
kusubiri taa iwaongoze au trafiki mwingine.