RAIS Jakaya Kikwete amewaomba Watanzania kuombea mazungumzo baina
yake na vyama vya siasa vya upinzani, ikiwemo vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Watanzania (UKAWA), yanayotarajiwa kuendelea Jumatatu ijayo,
yamalizike kwa umoja na mshikamano.
Kikwete alisema hayo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na wazee wa
mji huo, ambapo alisisitiza kuwa tangu awali aliweka msimamo kuwa yuko
tayari kufanya kila awezalo, kuhakikisha mchakato huo wa Katiba mpya
unaendelea kwa kuzingatia mshikamano na umoja.
“Niliombwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa vilivyopo
bungeni (TCD), John Cheyo, kuwa tulizungumze suala hili ili kupata
muafaka na kikubwa tuwe na mshikamano,” alisema Kikwete.
Alisema baada ya ombi hilo, alikutana na vyama hivyo Agosti 31, mwaka
huu mjini Dodoma ambako, walipeana kila mmoja jukumu la kulifanyia kazi
na kukubaliana wakutane tena Jumatatu Septemba 8, mwaka huu kwa
majadiliano na makubaliano zaidi.
“Mkutano ule ulikwenda vizuri, tulizungumza mengi na kupangiana kila
mtu kazi ya kufanya, ninachoomba kwa sasa Watanzania watuombee
tutakapokutana tena mazungumzo haya yatutoe hapa tulipo tuwe pamoja na
mshikamano,” alisema Kikwete.
Imani ya JK
Tangu vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi kutoka
nje ya Bunge Maalumu la Katiba na kususia vikao hivyo, Rais Kikwete
alisema pamoja na changamoto hizo, ana matumaini baada ya mjadala na
changamoto, Katiba mpya itapatikana.
Hata alipokuwa akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Marekani
kutoka maeneo ya Jiji la Washington D.C na majimbo ya Virginia,
Maryland, California na New York, alisisitiza nia yake ya kuona mchakato
huo unaendelea kwa amani na mshikamano wa Watanzania.
Rais Kikwete alinukuliwa akikiri kuwa mchakato wa Katiba umekuwa na
changamoto, lakini kwake mchakato huo ni sawa na barabara ndefu ambayo
haikosi kona.
Alisema kona katika mchakato huo zitakuwepo, lakini akasisitiza kuwa
yeye ni mtu anayeishi kwa matumaini na ni matumaini yake kuwa mchakato
huo utaendelea na hatimaye kufikia mwisho vizuri kama ilivyo matarajio
ya Watanzania wote.
Alisema pamoja na changamoto za mchakato huo, hata Serikali haina
wasiwasi na hali hiyo kwa kuwa ndiyo hali ya uendeshaji wa nchi ya
kidemokrasia.
“Najua kuwa maneno yamekuwa mengi lakini si ndiyo demokrasia ya wazi
inavyofanya kazi? Sisi katika Serikali hatuna wasiwasi na hali hiyo.
Ndiyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika nchi ambako demokrasia inafanya
kazi,” aliwahi kusema Rais Kikwete ambaye hivi karibuni, alikabidhiwa
Tuzo ya Kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika 2014.
Katiba na wananchi
Rais Kikwete alisema kuwa mchakato huo, kimsingi, unatakiwa kuongozwa
na ukweli kuwa Katiba inahusu wananchi wenyewe na maisha yao, na wala
siyo tu mchakato huo kuongozwa na mjadala wa idadi ya serikali mbili ama
tatu.
“Mchakato wetu kwa muda mrefu umekuwa ukihusu idadi ya serikali, ziwe
mbili ama ziwe tatu. Kwangu mimi, idadi ya serikali ni muhimu, lakini
naamini kuwa Katiba iwe ni kuhusu maisha yenyewe ya wananchi na ustawi
wao, mwelekeo mzima wa mchakato huo usiwe kuhusu idadi ya serikali tu,”
alisema.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni dhahiri kuwa yapo mengi ambayo
hayajakaa sawasawa katika mchakato mzima hasa kuhusu jinsi Katiba mpya
itakavyolinda maisha ya wananchi na kusaidia kuboresha ustawi wao.
“Naamini kuwa yapo mengi kuhusu Katiba ambayo hayajapata muda wa
kutosha wa kuyajadili katika Bunge Maalumu la Katiba. Kimsingi, Katiba
ni Katiba ya wananchi, ni Katiba kuhusu maisha yao na ustawi wao. Hili
jambo sijaona kama linaonekana sana katika mjadala wa Katiba,” alisema
mshindi huyo wa Tuzo ya Kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika 2014.