Katika
hali isiyokuwa ya kawaida bibi mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa
Miaka (65) ambaye hakujulikana jina lake wala makazi yake amenusurika
kuuawa na wananchi baada ya kudhaniwa kuwa ni mchawi.
Tukio
hilo lililoshangaza na kushtua wakazi wa wilaya ya Geita mkoani Geita
limetokea jana majira ya saa 3.30 asubuhi katika mtaa wa Tambuka reli
ikiwa ni kilomita chache tu kufika Stendi ya Magari madogo yanayokwenda
katika vijiji vya mkoa huo.
Akizungumzia
tukio hilo mmoja wa mashuhuda Joyce Mcherwa ambaye ni mfanyabiashara wa
eneo hilo alisema yeye alikuwa anafagia nje ya kibanda chake na
kushangaa mama huyo anaunguka kutoka angani bila kuwa na kitu chochote.
Alisema mama huyo alikuwa uchi wa mnyama amejifunga kitambaa chekundu kichwani na hirizi shingoni.
Joyce aliongeza kuwa mama huyo alikuwa hajitambui huku akihangaika kupaa tena kwa kurusha mikono yake na kupiga kelele za kuomba msaada wa kutaka kupewa maji ya kunywa.
Muda mfupi baadaye alikata kauli (hakuweza kuongea tena) na kukaa kimya kama bubu.
Kufuatia
hali hiyo shuhuda alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi
waliokusanyika na kutaka kumuua wakidai kuwa vikongwe kama hao wamekuwa
wakisumbua wananchi kwa kuwaroga.
Hata
hivyo baada ya wananchi kufika na kutaka kumuua kwa kumchoma moto
askari polisi wa kituo kidogo kilichopo katika stendi hiyo waliweza
kunusuru mama huyo na kumpeleka katika Hospitali ya wilaya ya Geita kwa
kuwa alikuwa ameumia kichwani.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita Adam Sijaona alikiri kumpokea
mama huyo na kuongeza kuwa ameumia kichwani kwa kuangukia jiwe lakini
alikuwa hajitambui wala alikuwa haongei na kulazwa wodi namba saba (7)
kwa ajili ya matibabu zaidi.
Jeshi
la Polisi Mkoani hapa limedhibitisha kutokea kwa tukio hilo na
uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kubaini chanzo chake.
Na Valence Robert-Malunde1 blog -Geita