MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, John
Shibuda amesema kwamba hajakihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo bali
amekosana na mfumo wa utumishi wa ndani ya chama hicho.
Akiwasilisha maoni ya wachache ya kamati
namba nane, Shibuda alisema anahudhuria Bunge Maalum la Katiba kinyume
na msimamo wake kwa sababu Ukawa walishindwa kumjibu juu ya uwakilishi
wa wakulima, wafugaji ambao yeye ni mlezi wake.
“Niliwauliza Ukawa tusipohudhuria kule,
je, nani atawawakilisha wakulima na wafugaji ambaye mimi ni mlezi wake?
Walishindwa kunijibu ndio maana nikaamua kuja hapa,” alisema Shibuda
huku akishangiliwa na wajumbe wenzake.
Mbunge huyo pia alikanusha tuhuma kuwa
amenunua chama na akasisitiza kuwa yeye ni mbunge bora kama walivyo
washambuliaji bora wa mpira wanapohamia timu nyingine wanaenda
kuimarisha safu ya ushambuliaji ili wapate ushindi.
Pia amewataka wajumbe wa kundi la Ukawa
ambao wako nje ya Bunge warejee kujiunga na wenzao, vinginevyo walieleze
sababu za msingi zinazowatoa nje ya mijadala muhimu inayoendelea
bungeni.
Shibuda, ambaye pia ni Mbunge wa Maswa
Magharibi, alisisitiza kuwa amehudhuria vikao hivyo kuwakilisha wakulima
na wafugaji wa Tanzania.
Kama kawaida yake akijinasibu kwa
misamiati na tamathali za semi za Kiswahili, Shibuda alisema kabla ya
kuazimia kwenda bungeni alikutana na viongozi wake wa Ukawa ambao ni
Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF) na James Mbatia
wa NCCR-Mageuzi.
Alisema kiukweli viongozi hao wa Ukawa
walishindwa kumpa majibu ya kuridhisha juu ya uwakilishi wa wakulima na
wafugaji na wavuvi.
“Niliwauliza nini faida ya huu Ukawa kwa
wakulima hawa ninaowaongoza, walishindwa kunipa jibu na wakabaki
wanang’aa-ng’aa,” alisema Shibuda ambaye ni mlezi wa Chama cha Wakulima
wa Pamba Tanzania (TACOGA).
Alisisitiza kwamba katika vikao vyake
binafsi na wakulima, walimkatalia kata kata asishiriki katika siasa za
Ukawa kwa sababu hawakuona faida zozote kutoka kwenye umoja huo
uliowekeza katika kususia kwenye vikao vya Bunge vya Katiba.
Kuhusu madai dhidi yake kwamba alikuwa
anatarajia kukihama Chadema, Shibuda alijibu kwa kutumia methali za
Kiswahili kuwa ‘Kuhama Msikiti si kuhama Uislamu na kukosana na Shekhe
si kuuhama Uislamu'.
Pia, alitumia fursa hiyo kueleza nafasi
yake kwa mafumbo akijifananisha na wanasoka mahiri wa duniani, akiwataja
kwa majina Messi, Ronaldo, Drogba, kwamba hata kuhama kwake kutoka
chama kimoja kwenda kingine ni kwenda kukiimarisha.