WATOTO
watatu wa familia moja, wakazi wa Nyankumbu, Wilaya ya Geita, mkoani
Geita, wamefariki dunia usiku wa kuamkia jana baada ya nyumba yao
kuteketezwa kwa moto uliowashwa kwa mafuta ya petroli na mtu
asiyefahamika.
Dada
mkubwa wa marehemu hao ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili
Sekondari Mwatulole na wazazi wao, walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo
ambalo chanzo chake ni ugomvi wa ardhi.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya hiyo, Dkt.
Adam Sijaona, alisema miili ya watoto hao imehifadhiwa hospitalini hapo.
Aliwataja
marehemu hao kuwa ni Reginald Robert (9), mwanafunzi wa darasa la nne
Shule ya Msingi Nyankumbu Mkombozi, Sophia Robert (6) aliyekuwa akisoma
darasa la kwanza shuleni hapo na Remijius Robert (4).
Majeruhi
ni Scholastica Robert (15), ambaye amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali
za mwili wake ambapo hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali
ya Rufaa ya Bugando.
Wazazi
wa watoto hao ambao pia walijeruhiwa katika tukio hilo ni Bi. Angelina
Gaspa (36), ambaye amelazwa hospitalini hapo akiwa na majeraha katika
mkono wake wa kulia, mgongoni, begani pamoja na Bw.Robert Remijius (45)
aliyejeruhiwa kichwani.
Akizungumza
kwa tabu akiwa wodini, Bi. Gaspa alisema siku ya tukio walikuwa
wamelala watoto wakiwa chumbani kwao ambapo ghafla alisikia watoto
wakipiga kelele na kusema ‘mama tunakufa’ na alipokwenda kuwaangalia,
akakuta nyumba inateketea kwa moto.
“Nilikuta
nyumba nzima ikiwaka moto, tulipiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa
majirani ambao walifika na kuanza kuvunja milango pamoja na ukuta ili
waweze kutuokoa.
“Mimi
na mume wangu tulijitahidi kuvunja tofali japo tupate sehemu ya kupita
na majirani walipofanikiwa kuvunja nyumba, tayari watoto wangu watatu
walikuwa wameteketea kwa moto,” alisema.
Aliongeza
kuwa, anaamini chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa ardhi uliokuwepo kati
yao na mkazi mmoja wa eneo hilo (jina limehifadhiwa) ambaye alifika na
kuchimba kisima katika eneo ambalo wao walilinunua kisheria lakini
alidai ni lake.
“Tunaishi
vizuri na majirani zetu, yote tunamuachia Mungu kwani hata tulipotaka
kumlipa ili aondoke katika eneo letu alikataa na mgogoro huu umedumu kwa
mwaka mmoja,” alisema.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Manzie Mangochie, alisema kitendo
hicho cha kikatili hakitavumilika na aliyefanya tukio hilo lazima
asakwe kwa nguvu zote ili aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria mara
moja.
Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Kalangalala, Bw. Hamad Hussein, alisema watu
waliofanya ukatili huo walitumia mafuta ya petroli kuyamwaga mlangoni
mwa nyumba hiyo na kusambaa vyumbani ukianzi katika chumba walicholala
watoto hao.
“Katika
eneo la tukio, tumekuta ndoo ya plastiki yenye ujazo wa lita tano
iliyotumika kuhifadhia mafuta hayo, tunaomba ushirikiano kwa wananchi
ili tuwatie mbaroni wote waliohusika,” alisema