ZAIDI ya waathirika 1,000 milipuko ya mabomu Mbagala, wameomba Serikali kuingilia kati na kuwasaidia, ili wapate fidia inayostahili kutokana na mali na vitu vyao vilivyoharibiwa wakati wa mlipuko huo Aprili 2009.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mbele ya baadhi ya
waathirika hao, Katibu wa Kamati ya Waathirika hao, Thomas Mbasha,
alisema baada ya ajali hiyo, walilipwa fidia ndogo na waliandika
malalamiko yao kwa njia ya maandishi kwa Serikali wakitaka kuongezwa
fidia, lakini hawajapata majibu mazuri.
“Tumeandika
barua kadhaa kwa Serikali tukiomba fidia zetu lakini hakuna
kilichofanyika. Tunahitaji Rais aingilie kati suala hili ili tulipwe
stahili zetu kabla hajaondoka madarakani,” alisema.
Mbasha alisema fidia walizolipwa awali, hazikulingana na thamani ya mali na vitu walivyopoteza wakati wa mabomu hayo.
“Inakatisha tamaa kusema haya mbele ya umma lakini ndicho tulichopewa na Sserikali kama fidia,” alisema huku akionesha nakala za hundi zikiwa na kiasi walicholipwa.
Baadhi ya hundi za malipo hayo kutoka Benki Kuu (BoT) zilikuwa za Sh 1,400; Sh 2,700; Sh 1,950 na Sh 4,900.
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Stephen Gimonge alisema Rais Kikwete alitembelea eneo
hilo na kuahidi kuhakikisha waathirika wanalipwa fidia inayostahili
lakini ahadi hiyo haijazaa matunda.
Wakizungumza
na waandishi wa habari, waathirika hao waliokuwa wamekusanyika katika
viwanja vya Shule ya Msingi Mbagala Kuu, wilayani Temeke walithibitisha
kupokea hundi zenye kiasi kidogo cha malipo ya fidia, huku wengine
wakiandikiwa kulipwa Sh 1,000.
Omary Mbonde ambaye ni mmoja wa waathirika hao, alithibitisha kulipwa hundi ya fidia ya Sh 1,950.
“Fedha hizo nimelipwa kama fidia kwa ajili ya nyumba yangu iliyoharibika pamoja na vitu vyangu vingine,”
alisema na kuongeza kuwa alipeleka malalamiko yake kwenye kamati, ili
apate fidia inayostahili lakini hadi leo hajapata chochote.
0 Comments