Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar limemkamata mfanyabiashara Abdallah
Ahmed Abdallah maarufu Machips (45), na fundi wa simu za mikononi,
David Eliakim Odingo (32) kwa tuhuma za kuhusika na matukio makubwa
yaliyowahi kutokea Zanzibar.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, (DDCI),
Salum Msangi alithibitisha kukamatwa kwa watu hao mnamo Septemba 19
mwaka huu akieleza kuwa wanaendelea kuhojiwa Tanzania Bara.
“Tumewakamata kutokana na tuhuma za kujihusisha na matukio makubwa
yaliyotokea Zanzibar na watafikishwa katika vyombo vya sheria mara baada
ya uchunguzi kukamilika,” alisema Msangi.
Alisema kwamba hali ya usalama kwa hivi sasa Zanzibar siyo mbaya
lakini haipo salama kwa wahalifu kwa vile jeshi hilo linaendelea na
operesheni yake ya kisayansi ya kuwatafuta na kuwakamata watu wote
wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, Msangi alisema kwamba Jeshi la Polisi linaendelea
kuwatafuta wote watakaoguswa na matukio ya uhalifu yaliyotokea Zanzibar
ikiwamo ya tindikali, milipuko na vitendo vya mauaji vilivyotokea katika
miaka ya hivi karibuni.
Kukamatwa kwa watu hao kumefanya idadi ya Wazanzibari waliokamatwa na
kufunguliwa mashtaka Tanzania Bara kufikia 24, baada ya kukamatwa kwa
viongozi wa dini wakiwamo wa uamsho ambao wanakabiliwa na mashtaka ya
kuhusika na vitendo vya ugaidi.
Habari za ndani zilizopatikana kutoka Jeshi la Polisi zinadai kuwa
fundi David anayefanya shughuli zake maeneo ya Darajani, mfumo wake wa
mawasiliano umebainika kuwa karibu na baadhi ya watu wanaoshikiliwa kwa
tuhuma mbalimbali za matukio ya uhalifu yaliyotokea Zanzibar.
Kabla ya kukamatwa kwa Machips alikuwa alifanya shughuli zake za
upigaji wa picha za mihadhara ya Kiislamu na harusi pia kuuza video zake
katika duka lake liliopo katika eneo la Kwahaji Tumbo.
Tangu walipokamatwa hadi sasa watuhumiwa hao hawajafikishwa
mahakamani kutokana na kuendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma
mbalimbali zinazowakabili.
mwananchi
0 Comments