SERIKALI imelitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuunganishia wateja umeme ndani ya siku kama watalipa kabla ya saa nne asubuhi.
Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga wakati akizungumza na menejimenti ya Tanesco mkoa wa Mwanza katika ziara yake ya kukagua miradi ya umeme.
“Baada
ya Februari mwakani, mtu akija akalipia huduma ya kuunganishiwa umeme
kabla ya saa nne asubuhi, saa nane mchana awe amefungiwa
umeme,”alisisitiza.
Alisema
ni vema mameneja wa vituo husika kuhakikisha mahitaji yaliyo muhimu ya
kutendea kazi yanakuwepo, ikiwa ni pamoja na nguzo za umeme na wale
ambao wanashindwa kuweka mahitaji hayo ili kuwahudumia wateja kwa
wakati, basi waachie ngazi.
Alisema
ni vema kila meneja kufanikisha kazi hiyo ya kutoa huduma kwa muda
unaofaa na kuongeza kuwa iwapo nguzo za umeme zipo na wateja amelipia,
ni vema isizidi siku tatu mteja huyo awe amewekewa nguzo na kufungiwa
umeme.
“Na
hili ni elekezo kwa nchi nzima. Kama kuna meneja hawezi, basi ni vema
kuacha kazi. Tunahitaji kila meneja ajue Tanesco tunataka kufanya kazi
kibiashara. Hawa wateja wanatuletea fedha, ni lazima tuwasikilize na
tuwahudumie,” alisema.
Aliongeza
kuwa Serikali imekuwa inajitahidi kuhakikisha inaboresha miundombinu ya
kila sekta na kwa hilo, Tanesco haina sababu ya mteja alipie huduma na
asipate huduma hiyo haraka.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alishangazwa na mradi wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) awamu ya kwanza kutokamilika katika wilaya ya
Ukerewe akihoji ni kwa nini wananchi wa wilaya hiyo hawajakamilishiwa
huduma hiyo wakati awamu ya pili iko mbioni kuanza.
Alisema
hali hiyo haikubaliki na kuongeza kwamba kama mkandarasi hawezi kazi,
ni vema mkataba wake ukasitishwa ili kazi hiyo apewe mkandarasi
mwingine.
“Kama
mtu hawezi kazi, mnakaa naye vipi? Ikifika mwishoni mwa mwaka huu
hajamaliza kazi, ni vema mkataba wake uvunjwe na apewe mtu mwingine,”
alisistiza.
Akijibu
kuhusu kuchelewa kwa huduma hiyo wilayani hapo, Meneja wa Tanesco Mkoa
wa Mwanza, Stella Hiza alisema mkandarasi aliyepewa kazi hiyo
alicheleweshewa malipo lakini tayari ameahidi kukamilisha kazi hiyo
ifikapo Desemba mwaka huu.
0 Comments