MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru wafanyabiashara watatu,
wakiwemo mume na mke, waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 13 na
miezi sita jela kwa sababu ya wizi wa Sh bilioni 1.1 katika Akaunti ya
Madeni ya Nje ya (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Walioachiwa huru ni mume Manase Makale na mkewe Edda Makale, na mfanyabiashara mwingine Bahati Mahenge.
Washitakiwa
hao waliachiwa mwisho wa wiki iliyopita baada ya Jaji Augustine Shangwa
kukubali rufaa iliyowasilishwa na wafanyabiashara hao kupinga hukumu
iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka jana.
Akisoma
hukumu hiyo, Jaji Shangwa alisema anawaachia huru wafanyabiashara hao
kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kabisa kuthibitisha mashitaka
dhidi yao.
Aliamuru
wafanyabiashara hao waachiwe huru mara moja na kutengua amri ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyowataka warejeshe fedha hizo mara
baada ya kutumikia kifungo.
Katika
rufaa, wafanyabiashara walikuwa wakipinga hukumu iliyotolewa na jopo la
mahakimu Sekela Mushi, Sam Rumanyika na Lameck Mlacha, wakidai kuwa
kulikuwepo na upungufu mkubwa wa kisheria na kihoja katika kuwatia
hatiani.
Katika
hukumu iliyotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahenge alitakiwa
kutumikia kifungo cha miaka saba jela, Makale kifungo cha miaka mitano
jela na mkewe Edda kifungo cha mwaka mmoja na nusu.
Aidha,
mahakama iliamuru baada ya kutumikia adhabu hiyo, Mahenge na Makale
warejeshe kiasi cha Sh bilioni 1.18 walichodaiwa kukiiba katika akaunti
ya EPA.
Washitakiwa
walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kutenda kosa,
kughushi nyaraka mbalimbali na kuziwasilisha sehemu husika na kuiba
fedha hizo.
Katika
kesi hiyo, wafanyabiashara hao walikuwa wameshitakiwa na wenzao Davis
Kamungu na Godfrey Mushi ambao waliachiwa huru katika Mahakama ya Kisutu
kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao
bila kuacha shaka.

0 Comments