Huku zikiwa zimepita saa chache tangu wawashuhudie mahasimu wao
kwenye mbio za ubingwa wa ligi ya Hispania Real Madrid wakipoteza kwenye
mchezo wao wa kwanza wa ligi kwa mwaka 2015 , Fc Barcelona walijikuta
wakikutana na kichapo kama cha wenzao Madrid baada ya kukubali kipigo
cha 1-0 mbele ya Real Sociedad.
Dalili za mwanzo mbaya kwa Barca zilionekana tangu mapema baada ya
beki wa kushoto Jordi Alba kujifunga mwenyewe kwa kichwa akiwa kwenye
harakati za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa toka upande wa kulia .
Bao hili lilidumu hadi mwisho wa mchezo huku Real Sociedad walio
chini ya kocha wa zamani wa Manchester United David Moyes wakikomaa na
kuwazuia Barcelona katika shambulizi walilopanga .
Wachezaji wa Real Sociedad wakishangilia baada ya beki wa Barcelona kujifunga .
Pamoja na ukweli kwamba wengi watashangazwa na matokeo haya , ukweli
ni kwamba takwimu hazikuwa na ishara nzuri kwa Barcelona kwani mabingwa
hawa wa zamani wa ulaya hawajawahi kushinda mchezo wowote kwenye uwanja
wa Real Sociedad Estadio Annoetta tangu mwaka 2008 ambapo katika michezo
mitano iliyopita walifungwa mara nne huku wakitoka sare mara moja .
Kipigo hiki kimewanyima Barcelona fursa ya kupanda kileleni mwa
msimamo wa ligi ya Hispania baada ya kuwashuhudia wapinzani wao Madrid
wakipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Valencia .
Kocha wa Sociedad David Moyes akiwa kwenye harakati za kuwaelekeza wachezaji wake kwenye mchezo dhidi ya Barcelona.
Benchi la Barcelona wakati wa mchezo dhidi ya Real Sociedad.
Kwa matokeo haya Real Madrid wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na
pointi 39 wakiwazidi kwa pointi moja wapinzani wao Barcelona wenye
pointi 38 sawa na mabingwa watetezi Atletico Madrid japo vijana wa Carlo
Ancelotti wana faida ya mchezo mmoja mkononi ambao endapo watashinda
wataomgeza tofauti ya pointi baina yao na wapinzani wake wa karibu kwa
pointi tatu zaidi .
Msimamo wa ligi ya Hispania kama ulivyo baada ya michezo ya wikiendi hii.
0 Comments