Mawaziri hao ni wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; William Lukuvi, Waziri
wa Maji; Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira.
Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za
Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira, wabunge hao walionekana kukerwa na ahadi zisizotekelezeka za
mawaziri hao kiasi cha wao kukata tamaa.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola akichangia
taarifa hizo aliwashukia mawaziri watatu kwa wakati mmoja akieleza
kuhusika kwao kukwamisha baadhi ya mambo.
Alisema migogoro ya ardhi nchini haitakwisha kama
viongozi ndiyo wanaohusika kulinda baadhi ya watu. “Wako viongozi
wanahodhi ardhi na kusababisha matatizo, mwekezaji wa Oysterbay Villa,
Lukuvi ndiye alimsaidia kupata eneo alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam,” alisema Lugola na kuongeza:
“Sasa leo amekuwa Waziri wa Ardhi, itakuwaje? Mimi
nitaichoma moto mbeleko inayombebea huyu mwekezaji kitendo kinachozuia
Kinondoni kupata Sh3 bilioni. Huyu mwekezaji ana kiburi alizuia hata
kamati kutaka kuingia kwenye eneo hilo lakini nikatumia ubaunsa wangu
tukaingia.”
Hata hivyo, hoja ya Lugola kuhusu Lukuvi na
mwekezaji huyo ilipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto
Kabwe ambaye alisema waziri huyo alisaidia hata kubadilisha mkataba wa
umiliki wa Oystebay Villa, hivyo amwache.
Lugola akiendelea kuchangia alimshukia Waziri
Maghembe kwamba anapeleka maji katika eneo lake tu wakati wananchi wa
jimbo la Mwibara na Bunda wakiteseka kwa mradi wao wa maji
kutokukamilika.
“Waziri alisema uongo hapa kwamba mradi
umekamilika kumbe ni uongo, niliwahi kuomba Rais atoe hawa mawaziri
mizigo na nimefurahi amefanya mabadiliko hivyo naomba yawe ya tija,”
alisema na kuongeza: “CCM isipigiwe kura hata mimi wasinipigie kama
mradi wa maji hautakamilika.”
Kuhusu Kilimo alieleza kuwa wanailinda Bodi ya Pamba na ndiyo maana kuna uchakachuaji mkubwa wa mbegu za pamba.
Alimtaka Nyalandu kwenda Mwibara kufanya mkutano na mamba na viboko ambao wanakula wapigakura wake huku akikaa kimya.
“Lazaro Nyalandu uende ukawazuie mamba na viboko
na kama unataka kwenda Ikulu halafu umeshindwa kuzuia mamba je, ukiwa
Ikulu utaweza kweli? alihoji Lugola.
0 Comments