Azam imeshinda mchezo huo dhidi ya Al Mareikh ya Sudan kwa matokeo ya 2-0 katika mchezo uliopigwa huko Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam ukishuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliojitokeza uwanjani humo kuishuhudia timu hiyo .
Azam walianza mchezo huo kwa kasi wakifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 8 mfungaji akiwa mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi Didier Kavumbagu aliyemalizia krosi ya Brian Majwega ambayo iliambatana na kosa la beki wa Al Mareikh.
Bao la pili la Azam lilikuja kwneye dakika ya 77 mfungaji akiwa John Bocco baada ya kufunga kwa kichwa akipokea pasi ya kichwa toka kwa Didier Kavumbagu ambaye aligusa mpira uliorushwa na Erasto Nyoni.
Azam walilazimika kufanya kazi ya ziada kwenye kipindi cha pili baada ya Al Mareikh kuwaingiza washambuliaji wake tegemeo Mohamed Traore na Augustine Okrah ambao waliongeza kasi ya mashambulizi.
Serge Paschal Wawa alikuwa nyota wa mchezo akiwazuia vilivyo wachezaji wa timu yake ya zamani Al Mareikh.
Timu hizi mbili zitarudiana wiki mbili zijazo huko nchini Sudan ambapo kama Azam wanahitaji kupata sare ya aina yoyote ile au kushinda ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya pili .
0 Comments