SERIKALI
imewataka wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu ambao bado
hawajapata ajira kutoa taarifa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
(HESLB).
Taarifa
hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia
Kabaka, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kasulu Mjini,
Moses Machali (NCCR-Mageuzi).
Katika
swali lake, Machali alitaka kujua Serikali inawasaidia vipi Watanzania
wanaodaiwa mkopo na Bodi ya Mikopo lakini hawana ajira mpaka sasa.
Kabaka
alisema mwanafunzi anapomaliza elimu ya juu hupewa mwaka mmoja wa
kujipanga na kutafuta kazi kabla ya kuanza kulipa deni lake.
“Baada
ya hapo kama anakuwa bado hajapata ajira atatakiwa kwenda kutoa taarifa
Bodi ya Mikopo kwa kuwa asipofanya hivyo akianza kulipa atalipa pamoja
na riba ya asilimia 10,” alisema.
Awali
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda
(Chadema), Naibu Waziri wa Kazi, Dk. Makongoro Mahanga, alisema jumla ya
mikopo iliyotolewa kuanzia mwaka 1994/95 hadi 2013/14 ni Sh trilioni
1.8 kwa wanufaika 291,582.
Hadi
kufikia Aprili 30, 2015 mikopo ya Sh bilioni 70.83 ilikuwa imerejeshwa
kwa wanufaika 136,803 kati ya wanufaika 177,017 ambao mikopo yao imeiva.
“Jumla
ya wanufaika 40,214 ambao wanadaiwa Sh bilioni 94.12 hawajaanza
kurejesha mikopo, jumla ya wanufaika 114,565 waliokopeshwa Sh bilioni
973.7 mikopo yao haijaiva hivyo haijaanza kurejeshwa kwa sababu
wanufaika ama bado wanaendelea na masomo vyuoni na wengine wako kwenye
kipindi cha matazamio,” alisema.
Katika swali lake, Mtinda alitaka kujua mpaka sasa Bodi ya Mikopo imeshakusanya kiasi gani na bado inadai kiasi gani.
0 Comments