MGOMBEA urais wa Tanzania anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amesema hana muda wa kujibu matusi na kejeli zinazotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi yake.
Badala yake amesema anatumia muda uliobaki wa kampeni kutafuta kura kwa wananchi kwa kunadi ilani ya chama chake.
Lowassa
aliyeteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyaeleza
hayo katika mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Mbezi Mwisho, jimbo la
Kibamba, jijini Dar es Salaam.
Kauli
hiyo aliitoa jana kama mrejesho wa kampeni ya kimkakati inayofanywa na
makada wa CCM walioamua kumshambulia wakimtuhumu kuwa hafai urais, ni
kapi, fisadi na mgonjwa.
“Sina
muda wa kuwajibu. Tukutane kwenye sanduku la kura. Katika siku 48
zijazo, mtaamua juu ya ajira za vijana, afya kama mtaendelea kulala
watano watano, mtaamua juu ya elimu yenu ambayo mimi natamani iwe bure
kuanzia msingi hadi chuo kikuu, maslahi ya walimu na viwanda vyenye
ajira,” alisema Lowassa ambaye tangu alipoanza kampeni amekuwa akiieleza Ilani ya Uchaguzi iliyopitishwa na UKAWA.
Lowassa
aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 25, na
kuzilinda kura kwa sababu tayari anazo taarifa kuwa CCM wamejipanga
kuiba kura.
Viongozi walianza kuhutubia saa 11:38 na kumaliza saa 12:10 jioni huku wananchi wakifika viwanjani hapo kuanzia saa 4 asubuhi.
Kulitokea
tafrani kidogo pale viongozi wasimamizi wa jukwaa walipoamua kuwaondoa
askari tisa wa Jeshi la Polisi waliofika mbele ya jukwaa kabla ya
viongozi kwa nia ya kutoa ulinzi. Ilielezwa kuwa viongozi waliona
“polisi hawaaminiki.”
Aidha,
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyejiunga na Ukawa wiki mbili
zilizopita, alisema CCM hawataki kuachia madaraka licha ya kutokubalika
kwa wananchi kwa sababu ya kudumaza maendeleo na kukumbatia rushwa na
kujikita kumshambulia yeye na Lowassa.
“Nasisitiza
watatoka tu, wamebaki na kazi ya kumchafua mgombea wetu na mimi.
Lowassa alitoka serikalini miaka minane iliyopita, hata Rais Jakaya
Kikwete alisema lililomkuta ni ajali ya kisiasa na kwamba hakuhusika na
Richmond. Kwa vile leo ametoka CCM anaonekana ni mbaya,” amesema Sumaye.
Akihutubia
jukwaani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliionya CCM na serikali
kuacha kuitumia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhujumu matokeo ya
uchaguzi mkuu.
“CCM
na serikali wanahofu. Baada ya kumchafua mgombea wetu pia wana mkakati
wa kuitumia TRA kuingiza bidhaa mfano mafuta bila kulipa ushuru ili
kuyauza na kununulia shahada za kupigia kura,” ametuhumu.
Mgombea
ubunge wa jimbo la Kibamba, John Mnyika alitumia fursa hiyo kujinadi
akisema Lowassa atakapochaguliwa kuwa rais atahakikisha serikali
inapeleka maji jimboni.
Mnyika
ambaye alikuwa mbunge wa Ubungo, jimbo linalogombaniwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), Saed Kubenea,
alimtaja aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Dk. Willibrod Slaa kuwa sasa ni
adui wa chama hicho.
Alisema
Dk. Slaa baada ya kukaa kimya kwa zaidi ya mwezi, tangu Chadema
kilipomkaribisha Lowassa kujiunga, ameibuka na kusema chama kimepoteza
misingi yake kwa kumpokea Lowassa na kumteua kugombea urais, hatua
inayoonekana ni ya makusudi ya kuinua CCM.
“Kuna
watu wametoka chooni wameingizwa chumbani… na mwingine ametoka chumba
cha Ukawa na Chadema ameenda chooni. Tatizo la msingi adui yetu mkubwa
ni CCM. Na sisi tunatangaza atakaeungana na CCM pia ni adui yetu,” amesema Mnyika.
Naye
Kubenea aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 25 kumpigia kura
Lowassa huku wakikumbuka wanapaswa kuondoa maradhi makuu matatu
yaliyotangazwa na Chama cha TANU (Tanganyika African National Union)
ambayo ni maradhi, umasikini na ujinga.
“Ili
Lowassa aweze kufanya kazi vizuri akiwa rais, lazima tupeleke wabunge
wengi wa Ukawa bungeni. Twende tarehe 25 Oktoba kupiga kura huku
tukikumbuka maneno ya rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyekaa madarakani
kwa miaka 10 bila ya kutuondolea upumbavu na ulofa,” alisema Kubenea.
Mkapa
alitoa maneno hayo jukwaani siku CCM ilipozindua kampeni yake kwenye
viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, alipolenga kumshambulia Sumaye,
waziri wake mkuu wakati alipokuwa rais.
Mpekuzi blog

0 Comments