Advertisement

Responsive Advertisement

Afariki Kwa Kuchomwa na Kisu Sehemu za Siri

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti mkoani Morogoro, mmoja wao kutokana na kuchomwa na kisu sehemu zake za siri alipokuwa akiamuliwa ugomvi wa kimapenzi katika Kata ya Dumila, wilayani Kilosa.
Akizungumzia aliyechomwa kisu, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema tukio hilo ni la Novemba 21, mwaka huu saa 6 usiku katika kata hiyo iliyoko Tarafa ya Magole . Alimtaja aliyeuawa ni Simon Paulo (19) mkazi wa eneo hilo na anayedaiwa kufanya mauaji hayo ni Frank Ziko (28) mkazi wa Kimamba, wilayani Kilosa.
Kamanda alisema, chanzo cha tukio hilo, ilisemekana ni wivu wa mapenzi kati ya mtuhumiwa huyo na mpenzi wake. Wakati Paulo (marehemu) akienda kuachanisha ugomvi huo, alichomwa kisu sehemu zake za siri na kusababisha kutokwa na damu nyingi na hatimaye kupoteza maisha.
Bila kumtaja mwanamke aliyekuwa na mtuhumiwa hiyo, Kamanda alisema mtuhumiwa amekamatwa na anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani. Wakati huo huo, Kamanda alisema tukio lingine la mauaji ni la Novemba 20, saa 3 asubuhi katika shamba la Stigmatine lililopo katika Kijiji cha Doronge , Kata ya Kisanga, Tarafa ya Mikumi, wilayani Kilosa.
Alimtaja aliyeuawa ni Laurent Mugale (52) aliyepigwa risasi moja shingoni upande wa kushoto. Kamanda alisema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi kati ya wanakijiji wa Doronge na Shirika la Stigmatine la Kanisa Katoliki .
Alisema trekta lenye namba za usajili T 150 DFN aina ya Massey Ferguson liliingizwa kulima eneo hilo na ndipo wananchi akiwemo aliyeuawa, wakilizuia lisilime hivyo kusababisha vurugu hali iliyosababisha mlinzi, Revocatus Anania (30) mkazi wa Dorogwe kufyatua risasi na kusababisha kifo.
Naye alijeruhiwa kwa panga katika bega lake la kushoto. Alikamatwa sambamba na walinzi wenzake watano kutoka Kampuni ya Bobbon na uchunguzi zaidi unaendelea.
Mpekuzi blog

Post a Comment

0 Comments